Thursday, August 21, 2014


Na  Nicasius Coutinho Suso

Simba wamevunja mkataba na kocha wao Logarusic. Ni huyu huyu waliokaa naye miezi sita ya mwisho wa msimu uliopita, ni huyu huyu ambaye walisema wamefanya uchunguzi wa kina na Kisha wakagundua kuwa anafaa kuwaongoza kwa misimu miwili ijayo, wakakaa naye chini akawaonyesha mipango, na namna atakavyoendesha timu Kisha wakakubali kuwa anawafaa na anastahiki mkataba huo.

Kwa kiwango cha Simba msimu uliopita haikuhitaji kuwa na kiwango cha kufikiri mithili ya mwanasayansi anayepanga kwenda mwezini au huitaji ujanja wa sungura kung'amua hili kuwa kwa mwenendo wa soka la Tanzania ni dhahiri huyu kocha asingekuwa na mkataba na Simba.
Katika Maisha ya kawaida ya mwanadamu ni rahisi kuufanya uongo kweli lakini Hapana shaka mwisho wa siku ukweli huja mahala pake, hata mwezi haukupita mpaka uongozi wa Simba chini ya Rais wao wakafanya kikao cha ghafla na kuutarifu umma na wapenzi wa simba kuwa hatokuwa kocha wa simba tena, na kuwa walijaribu kumvumilia lakini wameshindwa na haendani na matakwa ya klabu.
Rais wa Simba sc, Evans Elieza Aveva

Aibu ilioje, kama utafiti mliofanya wakati anaifundisha timu kwa kipindi cha miezi sita kiliwashawishi kumpa mkataba Leo utafiti wa wiki tatu umewapa Jibu tofauti? Hapa ndipo linapokuja lile Swala la soka la Tanzania na siasa za nchi, hata wafanyabiashara wamekuwa wanasiasa, wachezaji wanasiasa anagoma kwenda kucheza soka la ushindani kwa visingizio haba na mapenzi yasiyokuwa na msingi, na mwisho viongozi wa soka nao ni wanasiasa.
Na kwa vile Tanzania kwetu siasa ni uongo basi hata soka tunalifanya kiuongo na Ndo maana tunakubali kuwa Loga hajafanya vyema kiutendaji kwa wiki mbili baada ya kufanya vyema kwa miezi 6. Tunajaribu kuigeuza kandambili kuwa kiatu cha ujenzi.


Unamfahamu Martin Luther King? Mpigania uhuru na harakati za watu weusi kule Marekani, aliwahi kusema " Our lives begin to end the day we become silent about things that matter" alimaanisha Maisha yetu huanza kufika ukingoni tukiwa kimya kuhusiana na mambo ya msingi.

Na hapa ndipo tulipo, kufumbia macho mwenendo wa vilabu vyetu kutaendelea kuiteketeza jezi ya taifa pale uwanja wa taifa. Nasikia kocha wa timu ya taifa alisema Tofauti ilikuwa Pelembe, nasi tukakubali.
Alisema hivyo kwa sababu sisi ni siasa, anaamini miguu ya watanzania wote inahitaji mafunzo, anaamini Tanzania hatuna vipaji maridhawa hata gawa waliokuwepo akina Ngasa wanashindwa kuendelea kwa sababu wao ni wanasiasa na viongozi wanawadanganya kwa siasa, na kwa sababu anabaki ili awafunge simba na sie wapenzi wa soka tumeifurahia hii siasa. Ajabu sana ila ni kweli.


Wakati Aveva akifanya kikao na kuja na maneno ya kutuaminisha kuipenda Simba na ndio maana wamefikia hayo maamuzi wenzao Azam wapo mashindanoni, Yanga nao wakatuaminisha yale mashindano hayafai, bahati mbaya hata Coutinho wao ungemhoji angekujibu hayawafai siasa ya viongozi ishawaingia. Nchi za wenzetu zina utaratibu wa evaluation of the season.

Hapa yanapitiwa mambo yaliyoikuta timu, kiufundi, kibiashara na umaarufu. Hapa ndipo maamuzi hufikiwa. Sasa je Tanzania hatuna hili? Tanzania hatuna hesabu za tunavyopoteza? Tanzania tunajua kuingia mikataba? Najaribu kufanya hesabu za mikataba iliyovunjwa tangu mwaka Juzi kwa Mbiyavanga na wenzie, ubabaishaji wa Okwi mpaka Leo tunapomsema Loga.
Naamini Simba imepoteza kiwango cha pesa ambacho kingeweza kuwaweka vijana wao katika kambi bora na tungeanza kuwapata akina Pelembe sita kila msimu kutoka Academy. Lakini hakuna namna Aveva anaijua siasa, anazungumza maneno matamu mithili ya mzazi anayeleta pelemende baada ya kumchapa mtoto kiboko.
Na sasa ameng'ata  Kisha akapuliza wakati wadau wanajiuliza kuhusu Loga hajapoteza muda kamleta kipenzi Chao Phiri. Hawatoandaa mikutano wala maandamano ila wataenda airport kumlaki Kisha watamwita kiongozi bora. Kuna nyakati najiuliza hii namna ya viongozi hwa ya kishairi wanaitoa wapi? Wanazungumza kama washairi na wanatenda kama washairi.
Ngoja nami nikamsome Shabani Robert pengine itanisaidia kung'amua akili ya viongozi hawa, nasubiri Jaja, Maximo, na Coutinho upande wa pili nao,utakuja kishairi, nami wacha nijiandae kishairi kutabiri watakalosema.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog