Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
RATIBA ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa
2014/2015 unaotarajia kuanza kushika kasi septemba 20 mwaka huu ilianikwa jana
na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF.
Msimu ujao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa
hususani kuwania ubingwa ambapo klabu za Azam fc, Yanga, Mbeya City fc, Simba,
Kagera Sugar zinatabiriwa kuendelea kuwania nafasi tano za juu.
Lakini yanaweza kutokea mabadiliko kwa nafasi hizo
kwasababu Mtibwa Sugar, JKT Ruvu, Coastal Union, Ruvu Shooting zinaonekana
kijiandaa vizuri, hivyo timu zilizoshika nafasi tano za juu zisiwe na 100% ya kuendelea kuwepo.
Azam fc wamekuwa na utamaduni wa kuendeleza pale
walipoishia kama mambo hayatabadilika, lakini kwa Simba na Yanga wamekuwa
wakipokeza nafasi za juu mara zote. Kama Simba yuko katika kiwango cha juu,
basi utakuta Yanga wanasuasua, kama Yanga wako vizuri basi Simba wanakuwa ‘Mdobwedo’.
Lakini Simba na Yanga zote zinaonekana kuwa na nia
ya kutwaa ubingwa msimu ujao. Zimefanya usajili mzuri wa wachezaji, lakini
chachu nyingine imetokana na aina ya makocha waliopo kwa sasa.
Watakomaa msimu ujao?: Wachezaji wa Yanga wakiwa kwenye moja ya programu ya mazoezi ya Marcio Maximo.
Yanga wananolewa na Mbrazil, Marcio Maximo wakati
Simba wananolewa na Mzambia mwenye historia nzuri na klabu hiyo, Patrick Phiri.
Kwa upande wa Mbeya city fc si rahisi kutabiri
kwasababu wameshiriki ligi kuu kwa mara ya kwanza na kushika nafasi ya tatu,
lakini ni ngumu kujua kama wataendeleza
mafanikio hayo na kupanda juu zaidi.
Historia inaonesha kuwa Tukuyu Stars iliwahi
kupanda ligi kuu na kutwaa ubingwa mwaka 1986, lakini msimu uliofuata ikashuka
daraja. Kwa Mbeya City hawakuweza kufikia rekodi ya kutwaa ubingwa kama ‘Banyambala’,
lakini walijitahidi sana.
Kama wataendeleza pale walipoishia, basi watakuwa
na uwezo wa kushika nafasi ya pili au kubeba ubingwa.
Mtandao huu utakuwa ukikuchambulia timu moja baada
ya nyingine katika mechi zake kuanzia raundi ya kwanza mpaka raundi ya tisa
ambapo kutakuwepo na mapumuziko ya kupisha michuano ya ‘CECAFA Seniour
Challenge Cup’ na kombe la Uhai.
Leo tunaanza na wekundu wa Msimbazi Simba. Timu hii
inajengwa upya baada ya kuvurunda kwa miaka mitatu mfululizo.
Kwa mara ya mwisho kutwaa ubingwa ilikuwa msimu wa
2011/2012 chini ya kocha Mserbia Milovan Circovic. Kuanzia mwaka huo imekuwa
ikibadili makocha kila wakati.
Kutoka Milovan alikuja Mfaransa, Patrick Liewig, akafuata
mzawa Abdallah Kibadeni, Mcroatia Zdravko Logarusic na sasa Mzambia Patrick
Phiri.
Mabadiliko ya mara kwa mara ya benchi la ufundi ni
moja kati ya sababu kubwa zilizoiathiri Simba na kuondoka katika ushindani wa
ubingwa kwa muda mrefu sasa.
Lakini uongozi mpya chini ya Rais, Evans Aveva
umekusudia kuirudisha timu hiyo katika ushindani na kwa kuanza wameamua
kumchukua kocha aliyewapa ubingwa bila kufungwa mwaka 2009, Phiri, baada ya kuona Loga atawayeyusha msimu ujao.
Usajili waliofanya chini ya mwenyekiti wa kamati
ya usajili, Keptein wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania, (JWTZ), Zacharia Hans
Poppe umewapa matumaini zaidi ya kufanya vizuri.
Msimu ujao ratiba inaonesha kuwa mechi tatu za
kwanza, Simba watakuwa nyumbani uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Raundi ya kwanza itaanza Septemba 20 mwaka huu
ambapo Simba watachuana na Coastal Union.
Msimu uliopita, Simba walikuwa wazuri zaidi ya
Coastal United kwa kuangalia nafasi walizoshika kwenye msimamo. Simba walishika
nafasi ya nne wakati wagosi wa kaya walishika nafasi ya 9.
Kwa kuangalia takwimu hizi unaweza kusema Simba
watashinda mechi, lakini Coastal wamebadilika na wanaonekana kujifua vikali ili
kurudi na kasi mpya.
Kwa aina ya uchezaji wa Coastal, huwa wanawapa
ugumu sana Simba katika dimba la Taifa na hata msimu uliopita walishinda bao
1-0.
Kwahiyo mechi hii itakuwa ngumu kwa Simba, lakini
wana nafasi ya kushinda kutegemeana na namna Phiri atakavyokiandaa kikosi chake
na utayari wa wachezaji kupambana.
Raundi ya pili ambayo itakuwa septemba 27, Simba
watacheza na Polisi Morogoro uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Polisi Moro ni timu mpya, lakini huwezi kujua
wamejipangaje msimu ujao, Wamekuwa wakiendelea kujifua kila siku, lakini ugeni
wao pia utaweza kuwaathiri, ingawa imepita mwaka mmoja tu tangu washuke na
kupanda tena.
Mwalimu Rishard Adolf ni mzoefu na soka la ligi kuu na ndio maana kama unakumbuka baada
ya kuichukua Polisi mwishoni mwa msimu wa 2012/2013 alijitahidi kuisogeza
mbele, lakini alishuka daraja.
Mechi hii ya pili kwa Simba itakuwa ngumu, lakini
wana nafasi kubwa ya kushinda kutokana na uzoefu wao.
Raundi ya tatu, Simba watakabiliana na Stand
United kutoka Shinyanga, oktoba 4 mwaka
huu ndani ya uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. Kama Stand kweli watakuja na
moto waliokuja nao Mbeya City mwaka jana, mechi hii itakuwa ngumu sana kwa
Simba.
Lakini kutokana na ugeni wao, kuna vitu vya
kiufundi na kimbinu watazidiwa na Simba yenye wachezaji mchanganyiko. Lakini
mpira una vitu vingi, wanaweza kushinda, ila nadhani Simba watakuwa kwenye
nafasi kubwa ya kushinda kutokana na mazingira ya uwanja wa Taifa ambao utaweza
kuwaduwaza baadhi ya wachezaji wa Stand.
Baada ya kucheza mechi hizo tatu, raundi ya nne
Oktoba 4 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Simba watakuwa wageni
wa Yanga ya Marcio Maximo.
Hii itakuwa mechi ngumu kwa pande zote. Simba na
Yanga mechi zao hazitabiriki kirahisi. Timu bora inaweza kupoteza mechi au
kushinda.
Usitumie kigezo cha Yanga kuwa bora zaidi ya Simba
au simba kuwa bora zaidi ya Yanga na kutabiri timu fulani kushinda, wakati fulani
hesabu kama hizi huwa hazifanyi kazi inapofika mechi ya watani wa jadi.
Hata msimu uliopita ambao Yanga walikuwa wazuri
zaidi ya Simba, walishindwa kupata matokeo mechi ya mbili za ligi kuu ambapo
mzunguko wa kwanza walitoka sare ya mabao 3-3 na mechi ya marudiano walitoka
sare ya 1-1.
Wengi walijua Yanga wanashinda kutokana na namna
walivyosheheni nyota wengi tofauti na Simba, lakini Mnyama aligoma kuvutwa
sharubu na la kukumbuka zaidi ni jinsi alivyoweza kumcharaza Yanga kwenye mechi
ya Nani Mtani Jembe ambapo alishinda 3-1 mwezi desemba mwaka jana.
Baada ya kibarua na Yanga, raundi ya tano itakuwa
Oktoba 5, Simba watasafiri mpaka Mbeya kucheza mechi yao ya pili ugenini dhidi
ya Tanzania Prisons uwanja wa sokoine jijini humo, lakini itakuwa kama ya
kwanza kwasababu moja watakuwa wamecheza Taifa.
Sokoine ni miongoni mwa viwanja ambavyo si rafiki
kwa Simba. Simba wamekuwa wakihenyeka mno kupata ushindi mbele ya Prisons.
Licha ya Prisons kutokuwa katika ubora wake, mechi
hii itakuwa ngumu na nadhani sare ndio matokeo nanayoanza kutabiri, lakini
mabao pia yataweza kupatikana kwa timu yoyote.
Raundi ya sita Oktoba 26, Simba watakuwa uwanja wa
Jamhuri Mjini Morogoro kucheza na Mtibwa Sugar. Hii itakuwa mechi ngumu kwa
Simba na siwapi nafasi ya kushinda mbele ya wakata miwa, zaidi naamini sare
ndio yatakuwa matokeo rafiki kwa Simba.
Raundi ya saba itakuwa Novemba 2 ambapo Simba
watarudi nyumbani uwanja wa Taifa kukipiga na Ruvu Shooting. Hii itakuwa mechi
nyingine ngumu kwa Simba kutokana na Shooting kuendelea kubadilika.
Lakini kutokana na namna Shooting wanavyocheza
wakiwa uwanja wa Taifa ambapo hawaoneshi makali sana, nadhani Simba wataweza
kufanya vizuri ingawa sio lazima iwe hivyo.
Raundi ya nane, Novemba 8, Simba watacheza tena
uwanja wa Taifa dhidi ya Kagera Sugar. Hii itakuwa mechi ngumu sana kwa Simba
kutokana na uwezo mkubwa ambao huoneshwa na timu hii ya Kaitaba inapocheza
uwanja wa Taifa.
Raundi ya tisa itakuwa Novemba 16 ambapo Simba
watacheza ugenini dhidi ya Mgambo JKT
katika uwanja wa CCM mkwakwani.
Kwa kuangalia namna Mgambo walivyotumia uwanja wa
Mkwakwani hasa mechi za mzunguko wa pili msimu uliopita, unapata picha kuwa
Simba watahitaji kujipanga zaidi.
Baada ya raundi ya tisa kutakuwa na mapumziko ya
kombe la mataifa ya Afrika mashariki na kati na kombe la Uhai.
Mpaka kufikia raundi hiyo, Simba watakuwa wamecheza
mechi tano nyumbani. Lakini unaweza kusema sita kwasababu mechi na Yanga itapigwa
uwanja wa Taifa ambao unatumika na klabu hizo mbili kama uwanja wa nyumbani.
Kwa mazingira haya, kama Simba watatumia vizuri
uwanja wa nyumbani watakuwa wamekaa nafasi nzuri katika msimamo, lakini mpira
imebadilika, unaweza kufungwa kote kote.
Kesho tutaiangazia Yanga. Nawatakia siku mwema!
0 maoni:
Post a Comment