WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Halmashauri zitaelekezwa kwa waraka
ni vyanzo vipi vitahitaji kutumia wawakala wa ukusanyaji mapato kwani siyo kila
chanzo cha mapato ya Halmashauri kitakusanywa kwa ufanisi kwa kutumia au kwa
kutotumia mawakala.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo mchana (Alhamisi, Juni 30, 2016)
wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la 11 la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
Amesema katika ukusanyaji wa mapato, baadhi ya vyanzo vitapaswa
kukusanywa na Halmashauri zenyewe kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na
Serikali. “Moja ya miongozo hiyo ni kwamba kuanzia sasa, iwe kwa kutumia mawakala
au Halmashauri zenyewe ni lazima fedha zinazokusanywa ziwekwe kwenye akaunti ya
Halmashauri na kutumia mifumo ya kielektroniki ili kupunguza au kumaliza kabisa
masuala ya kutumia malipo kwa fedha taslimu (cash transactions),” alisema.
Amesema katika kutekeleza agizo hilo, Halmashauri itabidi zikubaliane na
wakala ni kiasi gani cha asilimia ya makusanyo kitalipwa kwa wakala na malipo
yafanyike baada ya kukusanya na kuingizwa kwenye akaunti ya Halmashauri.
Amesema Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura ya 290, inazipa uwezo
Mamlaka za Serikali za Serikali za Mitaa kutoza na kukusanya kodi, ushuru na ada
mbalimbali kama vyanzo vya mapato vya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Sheria hiyo pia inazipa mamlaka hizo kuteua mawakala wa kukusanya mapato
hayo kwa niaba ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu. Lakini Serikali imebaini changamoto za kiufundi katika kufanya
tathmini ya vyanzo vya mapato; ugumu katika kupata mawakala wenye weledi katika
ukusanyaji mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato, na wakati mwingine
watumishi wenyewe kujipa uwakala kinyume na taratibu zinazomzuia mtumishi
kufanya biashara na taasisi yake,” alisema.
Amesema hatua ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia mawakala ni
miongoni mwa mikakati ya kuboresha ukusanyaji mapato na pia kutoa muda mwingi
zaidi kwa watumishi wa mamlaka hizo kushughulika na majukumu ya msingi ya
Halmashauri na hasa utoaji wa huduma kwa wananchi na usimamizi wa miradi ya
maendeleo.
“Pamoja na dhamira nzuri ya hatua hizo, tunayo mifano ya baadhi ya
Halmashauri kama vile Nzega ambayo baadhi ya wahusika wameshinikiza wakitaka
zabuni zote wapewe madiwani. Jambo hili halikubaliki na tena ni kinyume cha
maadili ya utumishi,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote nchini kwamba kuanzia Julai Mosi, 2016
zihakikishe zinatumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato, katika
kulipa, kuweka na kutekeleza kikamilifu mikakati madhubuti ya kuboresha
makusanyo iwe yanakusanywa na Halmashauri au na wakala.
Amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa zina wajibu wa kutoa taarifa kwa
wananchi kuhusu mapato na matumizi ya Serikali pamoja na michango ya wananchi
licha ya kuwa uzoefu unaonesha kuwa mamlaka hizo zina tatizo la kukaa na fedha
kwa muda mrefu kabla ya kuzielekeza kwenye matumizi yaliyokusudiwa.
“Kuchelewesha kutoa fedha zilizotengwa kwa shughuli zilizopangwa ni
kuchelewesha kufikisha huduma muhimu kwa wananchi. Napenda kuhimiza uzingatiaji
wa utaratibu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mapato na matumizi ya fedha
za Serikali katika ngazi zote ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya
umma,” aliongeza.
Mkutano huo wa tatu wa Bunge ulioanza Aprili 19, 2016 ulikuwa mahsusi
kwa ajili ya kujadili na kupitisha bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya
Tano pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Bunge
limeahirishwa hadi Septemba 6, mwaka huu litakapokutana tena mjini Dodoma.
0 maoni:
Post a Comment