Na Saleh Ally
INAWEZEKANA
kabisa ikawa ni vigumu sana kwa watu wengi kuona ni miujiza kwa kampuni kubwa wanayoijua
kusikia imefeli na mwisho inafungwa kabisa. Yote yanawezekana ndiyo maana maduka
makubwa ya bidhaa maarufu kama Uchumi Supermarket, yamefilisika.
Biashara
inahitaji nidhamu ya juu sana, inahitaji kuwasoma wateja ambao sawa na
wamiliki, wanataka nini, kwa wakati gani lakini pia kusikiliza shida au kero
zao.
Mimi
siamini kama Kampuni ya DSTV imekuwa ikisikiliza kero za wateja wake hasa kwa
Tanzania, wengi wanalia na wako wameanza kuweka chuki kabisa.
Wote
wanaolia ni kuhusiana na bei, kwamba zimekuwa kubwa sana hadi kufikia kuona
kama ni sehemu ya kuwakomoa. Wako wanaoamini DSTV hawawajali wazalendo zaidi ya
kuangalia kile wanachoingiza.
Maoni
mengi huenda tumekuwa tukiyapata kwa kuwa wengi ambao wamekuwa wakiyatuma ni
watu wa michezo, wanajua Championi ndiyo makao makuu ya michezo kama
utazungumzia magazeti ya michezo, kweli hapa ndiyo nyumbani.
Wapenda
soka wengi hasa barani Afrika ni watu masikini, lakini mpira au soka ni zaidi
ya kabila na wengine ni zaidi hata ya dini, wanaupenda hadi kufikia kiwango cha
kuonekana kama wendawazimu.
Ndiyo
starehe kuu na tulizo la moyo, kama ukitokea kuwaingizia kero, hamtaelewana
milele. Ndiko hili suala linapokwenda, kwamba itafikia DSTV na Watanzania
wapenda soka au michezo wasiwe na urafiki hata kidogo.
Hii
inatokana na kilio cha malipo ya mwezi, hasa kwa wale wanaotaka kuangalia Ligi Kuu
England. Ili mtu apate nafasi ya kuangalia michezo ya moja kwa moja ya ligi
hiyo, basi lazima alipe takribani dola 100 (wakati mwingine ni zaidi ya Sh
200,000). Kwa Mtanzania wa kawaida hakika ni fedha nyingi sana.
DSTV
wanafanya biashara, hili hakuna anayeweza kukataa lakini bado kuna kila sababu
ya kuangalia mbinu za kibiashara na kuwapunguzia Watanzania kwa kuwa wanapenda
soka.
Nina
rafiki zaidi ya watatu ambao wameamua kuhamishia mapenzi yao Hispania.
Wanaamini La Liga ni bora kuliko Premier League lakini imekosa matangazo ya
kutosha. Wanaona DSTV sasa inaitumia EPL kama silaha ya kuwakandamiza wanyonge
na inawezekana kupunguzwa kwa bei.
KING'AMUZI CHA DSTV... |
Wanajua
kuwa Afrika Kusini kuna unafuu mkubwa wa bei ukilinganisha na hapa nyumbani
Tanzania. Wanaendelea kuamini La Liga ambayo sasa wanaweza kuipata kwenye
ving’amuzi vya Azam TV tena ikichambuliwa kwa lugha ya Kiswahili, itakata kiu
yao.
Nina
rafiki ambao sasa wanaangalia Premier League kupitia mitandao ambayo mtu
anaweka ‘bando’ yake ya intaneti na kuangalia moja kwa moja mechi hizo.
Hawa
ni wale wanaoondoka taratibu katika himaya ya DSTV ambao wanaona haiwezekani
lakini nawasisitizia kadiri siku zinavyosonga wanaotafuta njia mbadala watakuwa
wengi na watazidi kuachana nayo.
Azam
TV ambayo pamoja na gharama za uendeshaji kuwa kubwa kama DSTV wanavyosema,
lakini imejitahidi kuwapa Watanzania karibu kila kitu ambacho wanatoa DSTV na
huenda zaidi, lakini gharama ziko chini.
Hii
inafanya Watanzania wazidi kuongeza mapenzi na upande wanaoona unawajali. Najua
kuna gharama kubwa kupata uonyeshaji wa EPL lakini bado kuna njia zinaweza
kutumika kuwasaidia Watanzania katika suala la gharama za malipo ya mwezi.
Mara
zote, mtu anamjali anayemjali. Hata kama kweli wanafanya biashara, DSTV
wanatakiwa kuonyesha wanawajali Watanzania. Wajiulize, siku Azam TV wakipata
nafasi ya kuonyesha moja kwa moja mechi za EPL, wao itakuwaje?
0 maoni:
Post a Comment