Wafuasi
na wapinzani wa rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi
Wanafanya maandamano makubwa mjini Cairo mchana huu, huku waumini wa
dini ya Kiislamu wakiadhimisha Ijumaa ya kwanza ya mwezi mtukufu wa
Ramadan.
Wafuasi
wa Bwana Morsi wanatarajia kuwa mamilioni ya raia wa nchi hiyo,
wataendelea kuunga mkono wito wao wa kutaka Bwana Morsi kurejeshwa
madarakani.
Wapinzani
wa rais huyo wa zamani ambao waliandamana hadi rais huyo akaondolewa
madarakani na jeshi watakusanyika katika medani ya Tahrir.
Watu kadhaa wameuawa kwenye ghasia zilizotokea tangu Morsi alipoondolewa.
Mwandishi
wa BBC mjini Cairo, Jim Muir anasema vuguvugu la Muslim Brotherhood
huenda liliwatenga raia wengi wakati wa utawala wa Morsi, lakini bado
raia wengi wa nchi hiyo hawataki jeshi kuingilia masuala ya siasa.
Marekani kutuma ndege za kivita Misri
Siku
ya Alhamisi serikali ya Marekani, ilitoa wito kwa utawala mpya wa
Misri, kusitisha harakati zake za kuwakamata wanachama wa vuguvugu la
Muslim Brotherhood na kuonya dhidi ya kulenga kundi lolote.
Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon vile vile ameonya utawala huo wa
Misri kutotenga chama chochote cha kisiasa katika harakati za kutatua
mzozo wa kisiasa unaokumba taifa hilo.
Hata
hivyo msemaji wa Ikulu ya White House, Jay Carney amesema, utawala wa
Washington hauamini kuwa ni lazima isitishe misaada yake ya Misri.
Marekani
inatarajiwa kupeleka ndege nne za kivita aina ya F-16 nchini Misri,
lakini haijathibitisha kuwa msaada huo utatolewa lini.
Serikali
ya Marekani imesema, inachunguza ikiwa aumuzi huo wa jeshi la Misri
kumuondoa madarakani rais Morsi ni mapinduzi ya Kijeshi kwa kuwa sheria
za Marekani inazuia serikali kutoa misaada kwa nchi yoyote ambayo
kiongozi aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ataondolewa kupitia
mapinduzi.
Wafuasi
wa rais Morsi wamekuwa wakiandamana wiki nzima karibu na kambi ya
kijeshi iliyoko Mashariki mwa mji mkuu wa Cairo, ambako wanaamini kuwa
kiongozi wao anazuiliwa na maafisa wa kijeshi tangu alipoondolewa
madarakani
|
0 maoni:
Post a Comment