Wednesday, February 12, 2014


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), linatarajiwa kuendesha zoezi la ukaguzi wa katiba za wanachama wake ili kuhakikisha hazipingani na za Shirikisho la Kimataifa (Fifa), CAF na TFF. Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, kila mwanachama atawajibika kuwasilisha katiba yake na kisha kufanyiwa kazi na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya shirikisho hilo ili kubaini kama zina upungufu wowote.
“Katika kuhakikisha suala hilo linatekelezwa, mambo ya msingi yaliyomo kwenye katiba na kanuni za TFF, katiba za mfano za wanachama wa TFF zitapaswa kuingizwa katika katiba hizo kama vile, sifa za wagombea uongozi, ambapo zitaendelea kusomeka kama zilivyo kwenye katiba za mfano, kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF bila kufanyiwa mabadiliko,” alisema.
Mbali na hilo, Wambura alisema pia wanachama watatakiwa kuunda kamati zao za uchaguzi kwa kuzingatia kanuni za uchaguzi za shirikisho, ambapo kanuni za TFF ndizo zitakuwa mwongozo na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi wa Vyama Wanachama itakuwa ni Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF.
Kwa upande wa kamati za Maadili na Rufani za Maadili, alisema wanachama wa TFF wataunda kamati zao kwa kuzingatia kanuni za maadili za shirikisho, ambazo zitakuwa mwongozo, ambapo Kamati ya Rufaa ya Maadili ya Vyama Wanachama itakuwa ni Kamati ya Rufaa ya Maadili ya TFF.
Kuhusiana na leseni za klabu (Club Licensing), alisema kila klabu mwanachama wa TFF atalazimika kuingiza kipengele hicho kwenye katiba yake kutokana na maagizo ya Fifa na CAF.
Wambura alisema suala la muda wa ukomo wa madaraka, mwanachama atalazimika kuuweka katika katiba na kanuni zao za uendeshaji, kwa malengo ya kuhakikisha chaguzi zinaitishwa na kufanyika kabla ya muda wa Kamati ya Utendaji iliyoko madarakani kumalizika kikatiba, bila ya kujali sababu zozote zinazoweza kutolewa na mwanachama.
“Katika hili, TFF na wanachama wake hawatafanya kazi na kuitambua kamati yoyote ya utendaji ya mwanachama wake ambayo muda wake wa kukaa madarakani kikatiba umekwisha,” alisema.
Aliongeza kuwa pia kamati za muda, TFF na wanachama wake hawatazitambua na kufanya nazo kazi kamati zozote za utendaji ambazo hazikuchaguliwa na mkutano mkuu halali wa mwanachama wake.
Wambura aliongeza kuwa vyama vya mikoa na wanachama wa TFF, vinaagizwa kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa pia na wanachama wao ambao ni wilaya na klabu katika maeneo husika, na kwamba hakuna mwanachama atakayeruhusiwa kufanya uchaguzi kabla ya marekebisho ya katiba sambamba na uundwaji wa kanuni husika.
Alifafanua kuwa TFF itahakikisha hakuna mwanachama atakayetumia sababu hizo za marekebisho ya katiba kwa minajili ya kujiongezea muda wa kukaa madarakani.
Marekebisho hayo yanatakiwa kufanyika kabla ya Machi 20 mwaka huu na katiba ziwasilishwe TFF kwa uhakiki kabla ya kupelekwa kwa msajili.
Wanachama ambao watakuwa na matatizo katika mchakato huo, wawasiliane na TFF ili kupata mwongozo katika kufanikisha zoezi hilo.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog