Serikali
ya Afrika Kusini inachunguza uwezekano wa kuwasilisha ombi la kuandaa
mashindano ya Jumuiya ya Madola au Commonwealth mwaka wa 2022. Rais wa
kamati ya olimpiki nchini Afrika, Kusini Gideon Sam, amesema ana nia ya
kuomba mashindano hayo kuandaliwa barani Afrika kwa mara ya kwanza.
''Naamini huu ni wakati wa Afrika kuandaa mashindano hayo'' Alisema
Bwana Sam. Msemaji wa baraza la michezo nchini Afrika Kusini,
amethibitisha kuwa waziri wa michezo, Fikile Mbalula, tayari amepokea
ombi hilo na kuwa analiunga mkono. Akiongea na BBC, Sam, amesema kuwa
Afrika Kusini, ina uwezo wa kuanda mashindano hayo ya Madola kwa kuwa
taifa lake lina miundo mbinu ya kutosha na pia ujuzi wa kuandaa
mashindano mengine ya kimataifa.
Wizara
ya michezo nchini Afrika Kusini, sasa inatarajiwa kushirikiana na
kamati ya olimpiki nchini humo, kabla ya kuwasilisha ombi hilo rasmi kwa
baraza la mawaziri, ambalo litakuwa na uamuzi wa mwisho, ikiwa taifa
hilo linaweza kuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Afisa huyo amesema mji
utakaoandaa mashindano hayo utaamuliwa baada ya maafisa wa mabaraza ya
miji ya Durban, Cape Town na Johannesburg kuwasilisha rasmi maombi yao.
Bwan Sam vile vile ni naibu rais wa Kamati kuu ya mashindano ya Jumuiya
ya Madola, Commonwealth Games Federation (CGF), kamati ambayo inajukumu
la kuandaa mashindano hayo. Mwezi uliopita, CGF, ilielezea wasi wasi
wake kuwa hakuna taifa ambalo lilikuwa limeonyesha nia yake ya kuandaa
mashindano hayo mwaka wa 2022, huku muda wa mwisho kwa kutuma maombi ni
mwezi ujao. Hata hivyo nchi zinazodhamiria kuwa mwenye wa mashindano
hayo zimepewa hadi mwaka wa 2015 kutuma maombi yao.
0 maoni:
Post a Comment