Thursday, November 14, 2013

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
SIMBA SC inatafuta kipa mzuri wa kumsajili katika dirisha dogo, wakati huo huo inafikiria kuachana na kipa wake, Mganda, Abbel Dhaira ikibidi mapema iwezekanavyo au mwishoni mwa msimu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, kutokana na kanuni mpya ya usajili wa wachezaji wa kigeni msimu ujao ya wachezaji watatu kutoka watano, hawatahitaji kipa mgeni.
Tunatafuta kipa; Zacharia Hans Poppe amesema wanatafuta kipa wa kusajili dirisha dogo

Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba kwa sababu hiyo lazima waachane na Dhaira mwishoni mwa msimu, au kama atapata timu hata sasa ambayo itakuwa tayari kuilipa Simba, watamuuza.
Poppe amesema kwa sasa Simba SC tayari inasaka kipa atakayekwenda kuwa pamoja na makipa wa wazawa, Abuu Hasimu na Andrew Ntalla.
“Niseme wazi, tunatafuta kipa. Huu ni mchakato makini sana na hatutaki kurudia kosa. Tunatafuta kipa mzawa, kwanza awe mwaminifu na mwenye uwezo mkubwa,”alisema.
Kuhusu habari kwamba, klabu hiyo inabadilisha benchi la Ufundi, Poppe amesema kwamba huo si ukweli kwa sababu hakuna kikao chochote kilichoketi kujadili suala hilo.
“Ripoti ya kocha (ya mzunko wa kwanza wa Ligi Kuu) ndiyo kwanza inafika leo, wala hakuna kikao kilichoketi kuijadili, sasa hizo taarifa zinatoka wapi?”alihoji Poppe na kuongeza; “Sisi tunajua kuna hizo presha za kufukuza makocha, lakini hatujui haswa zinatoka wapi, mimi ninaomba nyinyi Waandishi muache kuvuruga wakati huu,”alisema.
Wakatu huo huo: Viongozi wa matawi yote Dar es Salaam wanatarajiwa wanatarajiwa kukutana makao makuu ya klabu Ijumaa asubuhi, kujadili marekebisho ya Katiba, mchakato unaoendelea vizuri hivi sasa klabu hiyo.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog