Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MAAFANDE wa JKT Ruvu wamekamilisha usajili wa
wachezaji watatu kati ya wengi waliokuwa wanafanya majaribio chini ya kocha
mkuu, Fredy Felix Minziro.
Beki wa kulia aliyeichezea Simba sc msimu uliopita,
Haruna Ramadhan Shamte amesajiliwa na maafane hao na kusaini mkataba mwa mwaka
mmoja.
Pia nyota wa zamani wa Simba sc na Azam fc, Jabir
Aziz ‘Stima’ ameanguka mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia klabu hiyo yenye nia
ya kuonesha changamoto kubwa zaidi msimu ujao.
Katika kuhakikisha lango lake linakuwa mikono
salama, klabu hiyo imemsainisha mlinda mlango mzoefu, Jackson Chove mkataba wa
mwaka mmoja.
Wachezaji hao watatu walikuwa chini ya uangalizi
wa kocha Minziro kwa muda mrefu kwa lengo la kujiridhisha na viwango vyao
pamoja na suala muhimu la nidhamu.
Jabir Aziz 'Stima'
Wachezaji wengine waliokuwa wanafanya majaribio na
klabu hiyo ni pamoja na Betram Mombeki na Henry Joseph, wote waliachwa na Simba
sc mwishoni mwa msimu uliopita.
Pia Athumani Idd ‘Chuji’ alijitokeza mara kadhaa
katika mazoezi hayo, lakini aliondoka zake baadaye na sasa anajifua na Mwadui
FC ya Shinyanga inayoshiriki ligi daraja la kwanza.
Meneja wa JKT Ruvu, Frank Joel Cibaya aliwahi
kukaririwa na mtandao huu akisema wachezaji wengi walioachwa na klabu kubwa za
Simba na Yanga wanaomba kufanya majaribio klabuni hapo, lakini kocha Minziro
yuko makini zaidi kuangalia nani anamfaa.
Jackson Chove
Cibaya alimtaja Aziz, Shamte na Chove kuwa
walionesha juhudi kubwa kwa muda wote wa uangalizi, hivyo kocha amependekeza
wasajiliwe rasmi kuitumikia klabu hiyo.
Meneja huyo alisema wachezaji wengi wanaotoka timu
kubwa huwa wanasumbua sana wanapojiunga na timu ndogo wakitaka kupata kila kitu
walichokuwa wanapata Simba na Yanga.
Dirisha la usajili limeongezwa kwa siku 10 hadi Agosti 27 mwaka huu, hivyo bado maafande wana nafasi ya kuongeza au kupunguza wachezaji wanaoona hawana manufaa kwao.
0 maoni:
Post a Comment