Mwalimu aliyetumia uchawi kuwaroga wezi, amejikuta akiwaroga shemeji zake waliopata uchizi
Butiama. Ilikuwa kama simulizi ya
kwenye filamu, baada ya mganga wa kienyeji aliyeletwa toka Kenya kuja
kuwaroga wezi walioiba nyumbani kwa Mwalimu mstaafu, Raphael Omwando
(60), baada ya dawa yake kuwatia uchizi ndugu wa mke mkubwa wa
aliyeibiwa.
Mwalimu Omwando ambaye ana wake wawili alivamiwa
na wezi waliomwibia pikipiki na mali nyingine, ikiwemo kumjeruhi yeye
(Omwando) na mkewe mkubwa. Mke mdogo aliyemuoa hivi karibuni anaishi
kwenye nyumba nyingine na hakuweza kuvamiwa na wezi hao, lakini mke
mkubwa alipigwa hadi kulazimika kupewa matibabu hospitali.
Watu walio karibu na familia hiyo walisema
kutokuelewana kati ya mke mkubwa na mdogo, kulimfanya mke mkubwa
aliyejeruhiwa na majambazi kumtuhumu mke mdogo kwamba alishirikiana na
majambazi hao.
Filamu hiyo ya familia ilianza kwa ndugu wa mume
(Omwando) wanaoishi Kenya, kuleta sangoma kwa ajili ya kubaini wezi
waliomwibia ndugu yao.
“Sijui nimefikaje hapa hospitali…maana kumbukumbu
zinaishia pale nilipolazimishwa kunywa dawa na mganga wa kienyeji
(Sangoma) anayedaiwa kutokea nchini Kenya …ili wezi wa pikipiki na vifaa
vya mwalimu mstaafu virudishwe,” hiyo ni kauli ya mmoja kati ya watu
wanne waliolazwa hospitali kwa madai ya kurukwa na akili.
Wagonjwa hao ni vijana wanne wa Kijiji cha Kirumi
Kata ya Bukanga, Tarafa ya Makongoro, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara
waliolazwa hospitali ya Mkoa wa Mara baada ya kunywa dawa hiyo na
kupoteza fahamu huku wakionekana kama mazuzu (Mazombi).
Waathirika
Matiko Joseph (25) anasema yeye alilazimishwa
kunywa dawa nyingi pamoja na makapi yake,” …Baada ya kumtajia mganga
hivyo akasema ninyi kunyweni nyingi…dawa ilikuwa na ukakasi
ilinikereketa sana. Baada ya kunywa niliondoka lakini baadaye hali
ikabadilika sana,” anasema na kuongeza,
“Nilishtukia niko hospitali tayari ikiwa ni siku
ya pili …Nikisimuliwa ilivyokuwa nazidi kushangaa…huyo mganga alilenga
kutuua kabisa….maana wakati anatoa dawa alisema atakayepata madhara
hatapona hata akipelekwa wapi mpaka vitu virudi ama fedha…akaondoka
kwenda Kenya na hakuacha simu wala jina lake kujulikana,” anasema Joseph
huku akipumua kwa harakaharaka.
Tura Joseph (30) anasema wengine walikunywa kidogo
lakini wao wana ndugu walilazimishwa kunywa zaidi kwa kile kinachodaiwa
kuwa walihisiwa kula njama za kumdhuru shemeji yao, na ndiyo
walidhurika zaidi.
Anasema baada ya kunywa alihisi kitu kinamkaba
shingoni na kuishiwa nguvu, akawa hoi na kuanza kuongea maneno
yaliyowatia shaka, ndugu wakawabeba kwa bajaji hadi hospitali.
Boniphace Joseph (20)huku akisitasita, anasema ana habari kabla
ya kunywa dawa lakini baada ya kunywa hakumbuki kilichoendelea mpaka
alipopata fahamu na kuona watu wanamshangaa naye akiwashangaa.
Msira Magesa (17) anasema yeye baada ya kunywa
alitoka kwenda kwenye shughuli zake, ghafla akazidiwa na kupewa dawa ya
kutuliza maumivu aina ya panadol hali ikazidi kuwa mbaya na kufikishwa
hospitali kwa matibabu
Hali ilivyokuwa
Julai 5, majira ya saa 5:15 usiku mwaka huu,
Mwalimu mstaafu, Raphael Omwando (60) alivamiwa na watu wanaodhaniwa
kuwa majambazi, wakamkata yeye, mkewe akapigwa na majambazi hao na baada
ya kipigo waliiba pikipiki, mabegi ya nguo, sola, sanduku dogo la
kuhifadhia nyaraka, simu ya mkononi na vitu vingine.
Omwando kutokana na majeraha aliyoyapata
akapelekwa hospitali ya mkoa alikolazwa kwa matibabu, lakini ndugu zake
wanaoishi Shirati na wale wanaoishi nchini Kenya baada ya kupata taarifa
waliamua kuchukua mganga wa kienyeji kutoka Kenya, ambaye
aliwahakikishia kuwa wahusika baada ya saa 3 watarudisha vitu
walivyoviiba wakiwa wamejitwisha na pikipiki wakiwa wanaisukuma.
Mganga huyo alieleza dalili za awali
zitakazowapata wezi hao kuwa ni kuchanganyikiwa, wengine watakuwa
wanakula nyasi kama ng’ombe. Mganga huyo alitoa tangazo kwamba Julai 9
majira ya saa 9:00 alasiri wanakijiji wote wajitokeze kunywa dawa hiyo
ili kuwapata wahusika.
Vituko vyao walikojoleana, kutapikiana
Mmoja wa wauguzi katika hospitali hiyo ambaye
hakutaka jina lake litajwe anasema, walipofikishwa hapo aliogopa,“
walikuwa wanakojoleana midomoni, wanatapikiana, huku wakiongea lugha za
ajabuajabu, tuliogopa maana ni tukio la kwanza kutokea,” anasema.
Anasema walipewa dawa za kuwafanya walale lakini
wakaonekana wanaendelea kuongea wengine kukimbia huku wakidai kuna watu
wanataka kuwaua, lakini sasa wametulia wanaongea wenyewe.
Shuhuda mwingine Isa Magesa anayemuuguza ndugu
yake anasema Matiko, mmoja wa waathirika hao alikuwa akikimbia kasi
kwenda nje huku akipiga kelele, “Nililazimika kutoa msaada,
nilipomkamata alionekana ana nguvu sana huku akisema…acheni kuniua…hao
wanakuja kuniua…nisaidie …wabaya hao, huku akionyesha kwa vidole lakini
wao hawawaoni,” anasema.
Mganga Mfawidhi.
Dk Iragi Ngerageza, Mganga Mfawidhi Hospitali ya
Mkoa, anasema vijana hao walifikishwa hapo wakiwa hawajitambui huku
ikidaiwa kuwa walipewadawa na mganga wa kienyeji na kuwapokea wakiwa na
hali mbaya na kuwa hali hiyo bado wanaendelea kuichunguza.
“Inakuwa vigumu kujua madhara ya hiyo dawa, kama tungeweza
kuipata na kupeleka kwa mkemia ingetoa majibu, lakini kwa sasa sisi
tunaendeleakuwatibu…lakini ni hatari maana kama walikunywa wakafikia
hatua hiyo lazima kuna kitu, ikipatikana itatusaidia,” anasema.
Mke wake akamatwa.
Pilly Esther mke mdogo wa Mwalimu Omwando
amekamatwa kwa kuhusishwa na tukio hilo, kusaidia kumpata mganga
aliyehusika na anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Butiama.
Hata hivyo akizungumzia tukio hilo anasema, wakati
mume wake anavamia yeye alikuwa kwake na alisikia kelele za mbwa,
lakini hakuelewa kilichotokea mwishoni akapigiwa simu na mke mkubwa kuwa
wamevamiwa na kuumizwa. “Ndugu wa mume wangu akiwemo mke mkubwa ambaye
ni Mjaluo wa kwao walinituhumu mimi kuwa ndugu zangu ndiyo wameiba mali
kwa kuwanimeolewa hivi karibuni..au mpenzi wangu wa zamani ndiye
amehusika, nilipokataa wakasema wanakuja na mganga kutoka Kenya
ambayeanatoa majibu haraka,” anasema.
Anasema mganga aliomba mtendaji kualika wananchi
wote lakini akakataa wakafika kama 40 wakiwemo kinamama, lakini kabla ya
kutoa dawa akawaanasema wahusika ni kama anawaona hapo anawaomba
wasinywe dawa, ajabuwaliopata madhara ni ndugu wa mke mkubwa.
0 maoni:
Post a Comment