Rais mstaafu, Benjamin Mkapa. |
Rais
mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameungana na wadau wengi wa
amani nchini, kutaka viongozi wa dini nchini kuendelea kuhubiri amani
ili kunusuru Taifa na matukio ya kuhatarisha amani ambayo yanaonekana
kuinyemelea nchi.
Mkapa alisema hayo jana jijini
hapa alipozungumza na maaskofu, mapadri na uongozi wa Chuo Kikuu cha
Weill Bugando wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika jengo
la maktaba ya chuo hicho, itakayopewa jina la Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere kama ishara ya kutambua mchango wake katika sekta ya
elimu wakati wa uhai wake.
Alisema siku za hivi karibuni,
Taifa limeshuhudia matukio ya kuhatarisha amani yakiwamo yale ya
waumini kuvamiwa katika nyumba za ibada, ambapo aliwataka viongozi wa
dini kuungana na Watanzania kuombea nchi iendelee kuwa na amani na
utulivu.
"Bila amani ni dhahiri nchi
itaingia kwenye matatizo, rai yangu kwa wananchi waendelee kuombea
viongozi wa dini waendelee kuhubiri amani na upendo katika Taifa letu,
naomba viongozi wetu wa dini waendelee kuhubiri amani," alisema.
Aliongeza kuwa uwepo wa amani
katika Taifa lolote duniani ni muhimu, kwa sababu itasaidia kuendelea
kufanyika shughuli za uzalishaji mali na ujenzi wa Taifa imara, kinyume
na hapo mipango ya nchi haitatekelezwa kikamilifu amani ikitoweka.
Aliushukuru uongozi wa Chuo
Kikuu cha Weill Bugando kwa kuamua kujenga maktaba hiyo, ambayo alisema
yeye wakati anasoma wazazi wake walimtaka asomee upadri, udaktari au
ualimu.
"Licha ya wazazi wangu
kunitaka niwe padri, daktari au mwalimu, nilijikuta nikisomea fani
zingine ikiwamo ya uandishi wa habari, lakini leo nafurahi kuungana
nanyi katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika jengo hili muhimu
kwetu sote," alisema.
Akiwa hapa, jana usiku Mkapa alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee ya ujenzi wa jengo hilo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
hicho, Padri Cleophas Mabula, alisema jengo hilo limejengwa kwa lengo la
kutekeleza azma ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania la utoaji elimu
bora katika fani za afya.
"Lakini pia ni kutokana na
ongezeko la wanafunzi chuoni hapa, ambapo kwa sasa chuo kina wanafunzi
1,536 kutoka 10 wakati kinaanzishwa mwaka 2003, hivyo tumeona kuna
mahitaji ya maktaba kubwa na ya kisasa," alisema.
Mabula alisema jengo hilo
linatarajiwa kuwa Kituo cha kujifunzia, huku likiwa na maktaba, kituo
cha Tehama, maabara zitakazokuwa zikiendeshwa kwa teknolojia ya Habari
na Mawasiliano na huduma nyingine pia.
Jengo hilo linajengwa na
mkandarasi Shirika la Uchumi la JKT-SUMA, kwa gharama ya Sh bilioni 3.4
fedha za ndani, huku kazi ya usimamizi ikifanywa na kampuni ya MK
ArchPlan Associates ya Mosh
0 maoni:
Post a Comment