Na Saleh Ally
KAMA ni Mwanaliverpool lazima utakuwa
unajua hadithi za wachezaji kama Phil Thomson, Graeme Souness, Alan Hansen
ambao waliifanya Liverpool kuanza kusimama katika miaka ya 1930 na baadaye
miaka ya 1970 na 1980.
Miaka hiyo ya 1980 kwenda 1990 wachezaji
kama akina Ronnie Whelan, Mark Wright halafu kikaja kizazi cha akina Ian Rush,
John Barnes na kumaliziwa na akina Paul Ince, Sammy Hyypia, Jamie Redknapp.
Najua watu wengi wa kizazi cha sasa
wanamjua zaidi Steven Gerrard, Jammie Carragher ambao walikuwa katika kizazi
cha mwisho kilichoiwezesha Liverpool kubeba Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya
wakiimaliza AC Milan katika mechi ya kihstoria mwaka 2005 jijini Istanbul,
Uturuki.
Katika mechi hiyo, hadi mapumziko,
Liverpool ilikuwa imetulizwa mabao 3-0. AC Milan waliona wamemaliza kazi,
lakini mpaka dakika ya mwisho, wakatoka vichwa chini.
Tangu mwaka 2005, baada ya Rafa Benitez
kuondoka Liverpool imeajiri makocha wanne na inaonekana imeshindwa kabisa
kurejea katika ukubwa wake inaoutaka.
Julai Mosi 2010 ilimuajiri Roy Hogdson,
ikamtimua Januari 2, 2011, hata mwaka haukutimia. Ikamwajiri Kenny Dalglish
siku hiyohiyo.
Dalglish ambaye ni gwiji wa Liverpool
alikaa hadi Mei 16, 2012. Tena ilionekana walimvumilia sana kwa kuwa ni mkongwe
wao. Hivyo, akakaa mwaka mmoja na miezi kadhaa. Nafasi yake ikachukuliwa na
Brendan Rodgers.
Juni Mosi 2012 ndiyo Rodgers alitua,
Oktoba 4, mwaka huu, naye kafungashiwa virago. Angalau amekaa miaka mitatu
lakini naye ameondoka mikono mitupu!
Kombe la mwisho la Liverpool ni lile
walilotwaa msimu wa 2011/12 chini ya Dalglish baada ya hapo, hata ngao tu
imekuwa hadithi na kumbukumbu kubwa zaidi hasa ukitaka kuzungumzia ya karibu ni
mwaka 2005 wakati Liverpool ikiwa chini ya Benitez ilipotwaa Kombe la FA, Ligi
ya Mabingwa Ulaya pia Uefa Super Cup.
Hii ni Liverpool ya ndoto za mchana!
Sasa imemwajiri Kocha Mjerumani, Jurge Klopp ambaye mafanikio yake yanajulikana
akiwa na timu ya Borussia Dortmund.
Klopp anauweza mzigo huu wa Mnyamwezi?
Tayari ameiongoza katika mechi mbili. Moja ya Ligi Kuu England, sare ya 1-1
dhidi ya Tottenham, pia sare kama hiyo katika Europa League dhidi ya Rubin
Kazan.
Mara ya mwisho Liverpool ilipopata
nafasi ya kusema ni wagombea ubingwa ni msimu wa juzi waliposhika nafasi ya
pili, tena waliokosa ubingwa kidogo wakati huo wakionekana kutegemea zaidi
nguvu ya juhudi za Luis Suarez. Msimu uliofuata, kaondoka kwenda Barcelona,
msimu huu Liverpool inaonekana taabani!
Klopp kweli ataweza kubadilisha kila
kitu kama ambavyo karibu kila shabiki wa Liverpool wa England, Tanzania na
duniani kote anavyosubiri kwa hamu?
Jibu hapana, Klopp hawezi kubadili kila
kitu ndani ya Liverpool ambayo inaonekana wazi kwamba ina matatizo mengi. Sawa
na kusema kumleta mziba pancha aongeze kasi ya gari ambalo linaonekana kutokuwa
na nguvu.
Mziba pancha hawezi kuongeza kasi ya
gari, ataziba pancha na kasi itabaki ileile. Kwa kuangalia kawaida tu unaona
Liverpool bado haina wachezaji wa kiwango cha kuiinua kutoka ilipo na kufikia
kiwango cha kuwa washindania ubingwa wa England au kurudi ndani ya Top Four.
Ukubwa wa Liverpool umebaki jina, lakini
ukweli kama atajitokeza mwekezaji na hasa wale wa kiarabu kama tulivyoona
Manchester City na Sheikh Mansour bin Zayed bin Sultan au PSG na Nasser
Al-Khelaifi, mchezaji tenisi wa zamani wa kimataifa wa Qatar kunaweza kuwa na
mabadiliko makubwa.
Kumekuwa na ambao wapo tayari kuinunua
na kuwekeza lakini Liverpool wenyewe hawataki hasa kwa wageni na wanaotokea nje
ya Ulaya. Kama hivyo, basi wakubali Warusi mamilionea ambao watakuwa tayari
kumwaga fedha zao na kuirekebisha.
Matajiri wa mafuta wanaonekana kuwa
tayari kumwaga fedha zao kama ilivyo kwa Roman Abramovich kutoka Urusi ambaye
ameigeuza Chelsea kuwa timu kubwa wakati haikuwa na umaarufu wa hivyo miaka 10
iliyopita.
0 maoni:
Post a Comment