Na Saleh Ally
LIGI Kuu Tanzania Bara msimu huu inaweza kuwa
ndiyo pekee au ya kwanza ambayo ina viwanja vingi vilivyofanyiwa ukarabati.
Siku za nyuma ligi hii huenda ndiyo ilikuwa ligi
kubwa zaidi Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyopigwa kwenye viwanja vyenye
viwango vya chini kabisa.
Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, Nangwanda Sijaona
(Mtwara), Ali Hassan Mwinyi (Tabora) na Samora (Iringa), vilikuwa kati ya
viwanja vyenye malalamiko makubwa kutokana na ubovu.
Ilionekana wazi kwa asilimia 90, viwanja vya Jiji
la Dar es Salaam pekee ndiyo vilikuwa na ubora unaowezesha angalau wachezaji
‘kuinjoy’ soka kutokana na ubora unaotakiwa.
Angalau CCM Kirumba ule wa Mwanza, uliendelezwa
ubora wake katika eneo la kuchezea. Hivyo kufanya ligi ionekane ni ya Dar peke
yake.
Si Chama cha Soka Tanzania (Fat) wakati huo au
klabu ambazo ziliamini suala la kurekebisha uwanja katika sehemu ya kuchezea ni
jambo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya soka nchini.
Asilimia kubwa ya viongozi wa Fat, hata baada ya
kubadilika kuwa TFF walionekana kujali zaidi suala la mapato. Waliangalia
wanaingiza kiasi gani cha fedha.
Upande wa klabu hali kadhalika, nao walionekana
pia kujali mapato katika mechi wanazocheza kwenye viwanja vyao na si sehemu ya
kuchezea uwanja zinakuwaje.
Hata wamiliki wa viwanja, mfano serikali au CCM
ambao wanamiliki viwanja kadhaa, bado walionekana zaidi wakijali mapato na si
wachezaji wanawezaje kucheza katika hali hiyo.
Hawakujali afya za wachezaji hao kutokana na
kucheza kwenye viwanja vyao hivyo vya kiwango cha chini kabisa! Bado hawakuona
kama ni sawa kuwa na viwanja bora vingesaidia kupanda haraka kwa ubora wa
viwango katika Ligi Kuu Bara.
Viongozi wa klabu, TFF na wamiliki wa viwanja
walikuwa tayari kutumia fedha zao hata kwa gharama kubwa kwa ajili ya
kuimarisha mageti ili wadhibiti mapato lakini si viwanja.
Kelele za wanahabari, naamini zilichangia
kupatikana kupatikana kwa mabadiliko kiasi fulani.
Mfano mabadiliko ya Uwanja wa Sokoine ambao miaka
nenda rudi, ulikuwa tatizo kubwa na ligi ilichezwa ukiwa una kokoto ndani yake,
jambo ambalo lilikuwa aibu kubwa kwa ligi kubwa zaidi Tanzania kuchezwa hapo.
Madaktari wa timu nyingi walilalamika kuhusiana
na uwanja huo na vingine lakini safari hii, Azam TV inaonekana kuyakimbiza
mabadiliko harakaharaka.
Azam TV imekuwa ikionyesha mechi za Ligi Kuu Bara
moja kwa moja au Live kama ilivyo maarufu. Hali hiyo imechangia kuonyesha ubovu
wa viwanja vingi tofauti na ilivyokuwa awali.
Kwa kuwa ni magazeti ndiyo yalipiga kelele sana
kwa kushirikiana na redio. Viongozi wa klabu, mashirikisho na wamiliki wa
viwanja waliweza kufanya propaganda kwamba havikuwa vibaya sana.
Utaona leo Uwanja wa Kaitaba wa mjini Bukoba
umetafutiwa udhamini na hivi karibuni uwekaji wa nyasi bandia utakamilika.
Kaitaba ulikuwa ukionekana kituko katika Ligi Kuu
Bara msimu uliopita. Marekebisho ya Uwanja wa Kambarage, Shinyanga wakijua
wataonekana live kwenye Azam TV.
Msimu uliopita, Mkwakwani mjini Tanga ulikuwa
tatizo. Mara baada ya msimu kwisha wakafanya marekebisho kuhakikisha sehemu ya
kuchezea iko bora, hilo limefanyika.
Kwa maana hiyo hakuna ubishi kwamba Azam TV
imekuwa ni sehemu ya mabadiliko ya haraka ya viwanja ambayo ni maendeleo ya
soka.
Angalau viongozi wa klabu leo wanaweza kuwahoji
wamiliki wa viwanja kufanya mabadiliko kutokana na muonekano unaokatisha tamaa
Azam TV inapoonyesha mechi live. Lakini hata TFF na Bodi ya Ligi
Tanzania (TPLB) nao wanaona haya sasa. Kwamba
ligi wanaoiongoza inaonekana kuchezwa katika sehemu duni kabisa huku wao
wakikunja mamilioni ya wadhamini ambao pia watakuwa wanahitaji ubora wa
muonekano ili kuthibitisha kwamba wanafanya kazi na watu makini wanataka
maendeleo ya dhati.
Huenda siku zinavyokwenda, mechi za moja kwa moja
kwenye Azam TV, zinaweza kusaidia kuwaamsha wadau wengi na kuusaidia mpira wa
Tanzania uzidi kupanda zaidi kimaendeleo.
0 maoni:
Post a Comment