Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro tayari imewasili salama nchini Uturuki katika mji wa Kartepe - Kocael leo mchana, tayari kwa kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika mwaka 2017.
Msafara wa Taifa Stars uliopoa nchini Uturuki unaongozwa na mjumbe wa kamati ya Utendaji ya TFF, Ahmed Mgoyi ukijumuisha benchi la ufundi 7 na wachezaji 21 umefikia katika hoteli ya Green Park Kartepe, ambapo leo jioni timu inatarajiwa kuanza mazoezi.
Kocha Mkuuu wa Taifa Stars Charles Mkwasa mara baada ya kufika katika eneo la kambi, amesema mazingira ya kambi ni mazuri na sasa vijana watapata nafasi nzuri ya kufanya mazoezi na kujiandaa vizuri kwa mchezo dhidi ya Nigeria.
Mkwasa amesema ana imani yeye na benchi lake la ufundi, wataandaa vijana kufanya vizuri kwa mchezo huo wa Septemba 5, 2015 na kuomba watanzania kuwaspoti katika maandalizi hayo kuelekea kwenye mchezo wenyewe.
Kwa mujibu wa ratiba ya kocha Mkwasa, timu itakua ikifanya mazoezi kutwa mara mbili kila siku uwanjani, na kutumia vifaa vya mazoezi viliyopo katika hoteli waliyofikia kuhakikisha timu ikirejea inakuwa katika hali nzuri ya kufanya vizuri zaidi.
Stars inatarajia kucheza michezo miwiliya kirafiki katika wiki moja ya kambi nchini Uturuki, kabla ya kurejea jijini Dar es salaam kupamabana na Nigeria.
TFF KUMPELEKA MAADILI MWENYEKITI WA UCHAGUZI DRFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatarajia kumpeleka katika kamati ya maadili ya TFF Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya DRFA Ndg. Rashid Saadallah siku ya Alhamisi tarehe 27/08/2015 saa 9:00 alasili kwa kosa la kudharahu na kupingana na maagizo ya mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya TFF.
Mwenyekiti wa kamati ya Uchaguzi ya TFF alimwagiza asimamishe uchaguzi wa chama cha mpira wa wilaya ya Temeke (TEFA), ili kuitisha fomu zote za waomba uongozi pamoja na maamuzi ya kamati za TEFA na DRFA ili kujiridhisha kama taratibu zilifuatwa katika mchakato huo kutokana na malalamiko ya baadhi ya wagombea kwamba hawakutendewa haki.
Pamoja na kupata barua hiyo kutoka kwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya TFF aliandika barua ya kukataa kutii maagizo hayo. TFF imechukua hatua hiyo kulinda nidhamu kwa vyombo vilivyo chini ya TFF.
U-15 YAINGIA KAMBINI
Kikosi cha timu ya Taifa cha vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U-15) kimeingia kambini katika hosteli za TFF zilizopo Karume kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya kombaini ya Morogoro (U-15) mwishoni mwa wiki hii.U15 inayonolewa na kocha wake Bakari Shime, ianatarajiwa kucheza michezo miwili na timu ya kombaoni ya Morogoro (U15) siku ya jumamosi na jumapili mjini Morogoro, ambapo kocha huyo amekua akitumia nafasi hiyo kupima uwezo wa vijana wake na kuboresha kikosi kwa kuongeza vijana wengine anaowaona wanafaa katika timu hiyo.TFF imekua na program ya timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 kukutana kila mwisho wa mwezi kwa kambi, kabla ya kusafiri mikoani kucheza michezo ya kirafiki. Mpaka sasa timu hiyo imeshacheza na timuza kombaini za mikoa ya Mbeya na Zanzibar.
Timu hiyo ya vijana wenye umri chini ya miaka 15, inajandaa na kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 nchini Madagascar mwaka 2017. IMETOLEWA NA TFF
0 maoni:
Post a Comment