Mgombea Urais wa UKAWA 2015 Edward Lowassa alianza ziara ya kuingia mitaani Dar es salaam Aug 24 2015 ili kukutana na Wananchi uso kwa uso na kusikiliza matatizo yao.
Lowassa amesema atatusaidia, tuna furaha sana leo ametutembelea, hatukutarajia,” alisema mwanafunzi wa Shule ya Nyegulu, Dorcus Wilson baada ya kuzungumza na Lowassa.
Mwanafunzi mwingine wa Shule ya Msingi Maarifa, Grey Issa alisema amefurahi kumuona Lowassa kwa sababu amekuwa akimwona kwenye televisheni. Alisema kero yao kubwa ni unyanyasaji wanaoupata kutoka kwa makondakta wa daladala.
Baadhi ya wananchi walisema Lowassa ndiye rais wao mtarajiwa kwa sababu haijawahi kutokea kwa kiongozi yeyote mkubwa kufika kwenye makazi yao na kuzungumza nao...
“Lowassa ndiye rais wetu. Ni mtu muhimu sana, amefika kwetu na kuzungumza na sisi. Angekuwa ni kiongozi mwingine angefika hapa na walinzi wengi,” alisema Augustino Nyembo, mkazi wa Gongo la Mboto.
Ilipotimu saa 2.35 asubuhi, waziri mkuu huyo wa zamani, aliingia kwenye daladala lililofika kituoni hapo kupakia abiria na kusafiri nalo kwenda Chanika. Baadhi ya abiria walistaajabu kumuona akiingia kwenye daladala hilo na baadhi yao waliteremka kwa mshangao.
Ndani ya daladala hilo, Lowassa aliketi kiti kimoja na mwanafunzi na muda wa kulipa nauli ulipofika, kondakta alisema; “Kwa kuwa wewe ni rais mtarajiwa sitakutoza nauli, utapanda bure”, ombi ambalo mgombea huyo alilikataa.
Lowassa alitoa noti ya Sh2,000 na kumtaka konda achukue nauli yake, pia akate ya mwanafunzi aliyekaa naye. Kondakta alichukua fedha hizo na hakurejesha chenji ya Sh1,400 wala kudaiwa. Watu wengine waliokuwa wameongozana naye katika daladala hilo walijilipia nauli ya Sh400 kila mmoja kutoka Gongo la Mboto mpaka Chanika.
Kondakta huyo, alimweleza Lowassa kuwa tatizo kubwa wanalolipata katika kazi yao ni kutokuwa na mikataba ya kazi na kwamba wanaweza kufukuzwa muda wowote bila kuwa na utetezi wa namna yoyote.
Mgombea huyo wa urais, pia alizungumza na wananchi eneo la Chanika na kuwasikiliza kisha kuendelea na ziara yake kuelekea Mbagala kwa kutumia gari lake.
Bodaboda wajiunga na msafara
Wakati msafara wa Lowassa ukielekea Mbagala, baadhi ya waendesha bodaboda waliufuata hadi uliposimama kwa ajili ya kujaza mafuta eneo la Kajiungeni.
Mmoja wa vijana hao, Zawadi Mrutu alisema wanampenda mgombea huyo kwa sababu ni mchapakazi na anaweza kuleta mabadiliko. Alisema hawajapewa fedha kujiunga na msafara wa Lowassa, bali ni mapenzi yao.
Alisema kiongozi wa wajasiriamali hao aliyezungumza juzi kwenye mkutano wa CCM hajui shida wanazozipata barabarani kwani kama angezifahamu... “asingezungumza vile. Hatumtaki tena kwenye chama chetu.”
Kijana mwingine, Ali Kasembo alisema wanachotaka ni mazingira mazuri ya kufanya kazi yao ya kusafirisha abiria. Alisema wamekuwa wakinyanyaswa na askari polisi katika kazi yao kwa madai kwamba wanakiuka taratibu.
“Lowassa ni jembe, namkubali sana. Tunataka atusaidie kupata mazingira mazuri ya kazi ili na sisi tuliojiajiri kwa kazi hii tujisikie huru, siyo kila siku tunakimbizana na polisi,” alisema Kasembo, anayefanya shughuli zake za bodaboda Chanika.
Akiwa Mbagala
Msafara wa Lowassa ulipofika eneo la Rangitatu, Mbagala na wananchi kumbaini, walianza kufuata gari lake huku wakiimba; “pisha, pisha, Rais apite…, pisha, pisha, Lowassa apite…”
Ilipotimu saa 4.05 asubuhi, msafara huo uliingia kwenye Kituo cha Daladala Mbagala Rangi Tatu huku watu wakisukumana kutaka kumuona.
Hata hivyo, Lowassa alipojaribu kuzungumza nao hakusikika kutokana na kelele zilizotawala kituoni hapo.
Baada ya spika kufungwa kwenye gari, mgombea mwenza, Juma Duni Haji alisimama na kusema wamepita kuwasalimia wale ambao wameitwa malofa. Alisema hatazungumza zaidi kwa sababu wataambiwa walifanya mkutano usiotambulika rasmi.
“Leo tumepita kuwasalimia maskini wanaoambiwa ni vibaka, malofa, wapumbavu. Tunaomba mtuache tuendelee na safari, tutakutana Jumamosi,” alisema Duni na kurejea kwenye gari na kuendelea na safari yao.
Mwenyekiti Monduli ahamia Chadema
Wakati huohuo; Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Arusha, Reuben Ole Kuney ametangaza kujiondoa CCM na kujiunga na Chadema.
Ole Kuney ambaye aliwahi kuwa mkuu wa wilaya mbalimbali kabla ya kustaafu, alisema amejiondoa CCM kutokana na kubaini chama hicho kimeshindwa kusimamia taratibu na kanuni zake.
“Mimi kama mwenyekiti wa wilaya anayotoka Lowassa, waziri mkuu wa zamani na mbunge wetu, siwezi kubaki CCM kwani chama kilishindwa kutenda haki katika mambo mengi ikiwamo mchakato wa urais,” alisema.
Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Elisante Kimaro alisema kamati ya siasa ya chama hicho itakutana Jumatatu kujadili mwenendo wake na kupanga ratiba ya kampeni.
0 maoni:
Post a Comment