Friday, July 3, 2015


Na Saleh Ally
ULIMSIKIA yule mchezaji kinda wa Yanga, Geofrey Mwashiuya aliyesema kwamba hata Yanga anapita, yuko njiani kwenda Ulaya ambako amekuwa na ndoto ya kucheza soka la kulipwa?


Mwashiuya ambaye amejiunga na Yanga msimu huu akitokea timu ya daraja la kwanza ya Kimondo, aliyasema hayo mbele ya waandishi wa habari kwamba Yanga anapita!

Kinda huyo ambaye ameonyesha kuwa ana kipaji hadi kuzua gumzo, aliwaambia Kimondo kwamba wamuache acheze Yanga badala ya kuendelea kulumbana, lakini akawa mstaarabu na kutoa shukurani kwao kwa kumlea katika kipindi cha misimu miwili alichoichezea timu hiyo.

Baada ya hapo, ndiyo akatoa kauli hiyo kwamba Yanga anapita. Yeye ndoto yake imekuwa ni kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.

Kweli wachezaji wengi Watanzania wamekuwa na ndoto za kucheza soka la kulipwa barani Ulaya lakini kuzungumza tu imekuwa shida na hiyo ni sehemu ya kuonyesha kwamba hawajiamini.

Wengi wamekuwa wakizungumzia ndoto zao baada ya kustaafu. Utasikia: “Nilikuwa na ndoto ya kucheza Ulaya lakini hata hivyo mambo hayakwenda vizuri. Wakati wetu pia ilikuwa shida sana!”

Unawajua wachezaji wangapi ambao wanaona kuchezea Yanga au Simba ndiyo mwisho wa safari? Wanaona kufikia kuchezea timu hizo, basi hakuna sababu tena ya kuendelea kutafuta kwingine.

Kweli Yanga na Simba ndiyo klabu kongwe na zenye mashabiki wengi zaidi lakini hakuna ubishi ni lazima kwa mchezaji yeyote bora kuvuka mipaka ili kutafuta mafanikio zaidi.

Kwangu alichokisema Mwashiuya kinaonyesha namna alivyo na moyo mpana, namna alivyo na pumzi ya kutosha kwenye ubongo wake na anavyoweza kufikiria mambo mengi na kutaka kuyafanyia kazi.

Huenda anaweza kuwa mchezaji wa kwanza au wa mwisho kusema Yanga anapita akiwa hata hajapata uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza.

Wengine wote wangezungumzia namna wanavyoweza kupata nafasi katika kikosi cha kwanza na kuitumikia Yanga kwa nguvu zote ikiwezekana kuisaidia kuipa ubingwa.

Kauli ya “Yanga napita”, ina mengi ambayo yamejumlishwa zaidi na yale ambayo yangeweza kusemwa na wengine kwani inaonyesha ili apite Yanga, lazima afanikiwe. Ili afanikiwe lazima ajitume, apate namba ya uhakika, aisaidie Yanga kufanya vizuri halafu aonekane.

Kwangu namuona ni kijana jasiri sana. Nilisoma makala ya Edibily Lunyamila katika Gazeti la Championi la juzi akimueleza kinda huyo mambo mengi ikiwa ni pamoja na kutolewa sifa mapema ambazo zimewaangusha wengi sana.

Sioni sababu ya kuyarudia yote ambayo Lunyamila alimueleza Mwashiuya, lakini ukweli yalikuwa ni sehemu ya maneno bora ambayo anaweza kuyachukua na yakasaidia kumjenga na kumfanya awe imara katika safari yake ya kuiwinda Ulaya.

Kikubwa ni kumpa ushirikiano, kama kipaji chake kinafanya kazi basi aungwe mkono kwa kuwa akishatoka nje ya Tanzania, hatakuwa wa Yanga tena, badala yake atakuwa ni mchezaji kutoka Tanzania na kwa faida ya taifa letu ambalo linahitaji wachezaji wengi waende nje ya Tanzania.

Kikubwa ambacho ninaweza kumkumbusha ni kwamba safari hiyo ya kwenda Ulaya haiwezi kuwa rahisi au laini kama ambavyo anafikiria. Kuna milima na mabonde na haitakuwa rahisi kwa kuwa si kila mmoja hata wengine walio Yanga watafurahia yeye kuona anakwenda Ulaya.

Dunia ina watu tofauti sana, wenye husda, wenye roho mbaya na wasiopenda maendeleo ya wengine. Mara zote huwa wanazidiwa nguvu na ukweli na hasa kama yeye atafanya kazi yake akiwa ana malengo kweli ya kuvuka na kufika anapotaka kwenda.

Kumuomba Mungu ni jambo muhimu katika kila kitu, lakini Mwashiuya lazima akubali kwamba utulivu wa akili, kujituma na nidhamu ya hali ya juu ni baadhi ya mambo muhimu yatakayomfikisha katika ndoto yake ya kupita Yanga na kwenda kucheza Ulaya.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog