TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 20, The Tanzanite, imeanza vibaya mbio za kuwania tiketi ya fainali za Afrika, baada ya jana kufungwa mabao 4-0 na Zambia Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Ilikuwa huzuni kwa Watanzania wote waliojitokeza Uwanja wa Azam, Chamazi wakiongozwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi namna ambavyo Tanzanite walivyonyanyaswa na mabinti wenzao shupavu wa Zambia.
Tanzanite inayofundishwa na mzalendo, Rogasian Kaijage leo ilizidiwa kabisa na Shepolopolo Uwanja wa Azam na kujikuta hadi mapumziko ikiwa tayari imekwishabugizwa 3-0.
Mabao ya Shepolopolo yalifungwa na Memory Phiri dakika ya nne, Irene Lungu dakika ya 20 na Barbara Banda dakika ya 33.
Kipindi cha pili, Zambia walirudi na moto wao tena na kufanikiwa kupata bao la nne, mapema tu dakika ya 50 kwa penalti kupitia kwa Marry Wilombe.
Refa Batouli Ibrahim wa Sudan alitoa penalti hiyo baada ya Anastazia Anthony kumfanyia faulo mshambuliaji wa Zambia, Memory Phiri.
Sasa Tanzanite inatakiwa kwenda kushinda mabao 5-0 ugenini ili kusonga mbele.
Kikosi cha Tanzanite: Najjiat Abbas, Zuwena Aziz, Happiness Hezron, Maimuna Hamisi, Anastazia Anthony, Donisia Daniel, Hamisa Athumani, Neema Paulo, Asha Shaaban Hamza/Janet Cloudy (dk 40), Shelider Boniphace na Stumai Abdallah.
Zambia: Hezel Natasha Nali, Mary Wilombe/Osala Kaelo (dk 75), Margaret Belemu, Martha Tembo, Mlika Limwanya, Lwendo Chisamu, Esther Mukwasa, Irene Lungu, Grace Chanda, Barbara Banda na Memory Phiri/Agnes Musesa (dk 83).
0 maoni:
Post a Comment