Thursday, March 5, 2015


Madhara ya mvua hiyo

Mbunge wa Jimbo la Msalala Mheshimiwa Ezekiel Maige
  • Kufuatia tukio la kusikitisha na kuhuzunisha lililotokea usiku wa kuamkia Machi 4,2015 huko katika kata ya Mwakata wilayani Kahama mkoani Shinyanga la watu 42 kupoteza maisha na wengine 91 kujeruhiwa kutokana na mvua kubwa iliyokuwa imeambatana na upepo na mawe,mbunge wa Jimbo la Msalala kulikotokea tukio hilo,Mheshimiwa Ezekiel Maige,amezungumzia tukio hilo.

    Alichokisema hiki hapa chini:






Nimepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za mvua kubwa, yenye upepo na theluji nyingi iliyonyesha kwa muda wa dakika 35 tu saa 5 usiku wa kuamkia leo Jumatano Machi 4,2015.


Nimepata taarifa za tukio hilo nikiwa safarini Kigoma kikazi na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa ambayo mimi ni mjumbe.


Kutokana na uzito wa tukio hili nimesitisha ziara hiyo na kuondoka Kigoma majira saa 5 asubuhi na hivyo kufika Mwakata saa 2 usiku huu.


Hali niliyoikuta kama wengi walivyokwishatoa ushuhuda ni ya kusikitisha na kushangaza sana.


Sijawahi kuona maafa yatokanayo na mvua katika jimbo langu miaka yote niliyoishi hapa.


Maafa ni makubwa yasiyoelezeka.


Naomba kusema yafuatayo:-


Kwanza, nawapa pole sana familia zote zilizopoteza wapendwa wetu. 

Mungu awarehemu wapendwa ndugu zetu waliopoteza maisha katika tukio hili. 

 Aidha namuomba Mungu atupe moyo wa ujasiri kuikabili hali hii na atupe nguvu za kusimama haraka na kurejea kwenye hali ya maisha yetu ya kawaida.

 Pia namuomba Mungu atuepushe na mitihani ya kiwango hiki ambayo kwa kweli ni mizito.


Pili, nawashukuru sana viongozi wa serikali na Chama, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya maafa wilaya ya Kahama ambaye ni mkuu wa wilaya ya Kahama  Benson Mpesya kwa juhudi kubwa walizofanya kuokoa majeruhi na kusaidia wahanga. 

Wamefanya kazi kubwa sana kwani, hadi jioni nilipofika kwenye eneo la tukio, majeruhi wote 91 walikuwa wamefikishwa hospitalini na walikuwa wanaendelea kupata matibabu na miili ya marehemu kadhaa ilikuwa imeanza kuzikwa. 

Aidha nawashukuru kwa kusaidia vitu mbalimbali ikiwemo vyakula.


Tatu, nawashukuru sana watu wote wenye mapenzi mema ambao wameanza kutupatia misaada mbalimbali ikiwemo unga, mablanketi, sukari, mikate na vinywaji mbalimbali.

 Nawaomba watu wote wenye mapenzi mema waendelee kusaidia kwani waathirika ni wengi, zaidi ya 4,000 hivyo hali itazidi kuwa mbaya jinsi siku zitakavyosonga mbele endapo ndugu zetu hawatapatiwa msaada.


Nne, mimi kama Mbunge wa eneo husika, pamoja na kusikitishwa na tukio hili, natoa wito kwa serikali, hasa Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa, makampuni, taasisi, mashirika na watu binafsi wasaidie kwa haraka misaada ya chakula, mavazi na makazi kwa waathirika. 

Binafsi nitawasilisha msaada wangu wa tani 5 za unga kesho asubuhi tarehe 5,Machi ,2015 .


Tano, naomba sana watu wote wenye mapenzi mema wasaidie kurudisha maisha ya waathirika kwenye hali ya kawaida hasa kwa kuwasaidia vifaa vya ujenzi kama mbao, bati na theluji.


Sita, ombi maalum kwa serikali, naomba sana serikali itoe punguzo maalum la ushuru kwenye simenti, nondo na mabati kwa wananchi wote wa Kahama ambao wengi wao wana nyumba za tope zilizoezekwa kwa nyasi, na hivyo kutokuwa imara kuhimili upepo mkali au mvua kubwa.

 Inavyoonekana, mabadiliko ya tabia nchi sasa ni dhahiri kwamba matukio ya kimbunga au mvua kubwa zenye upepo yanazidi kuongezeka Kahama, kwani ni wiki moja tu imepita tangu mvua yenye upepo iliponyesha kwenye kijiji changu cha Segese ambapo nyumba zaidi ya 50 zilianguka au kubomoka na nyingine nyingi kuezuliwa mapaa. 

Tukio hilo liliathiri hata nyumbani kwa mzazi wangu ambapo ukuta wa uzio ulianguka!


Ukiangalia maeneo yaliyoathirika, idadi kubwa ya nyumba zilizoanguka ni nyumba za tope zilizoezekwa kwa nyasi.

 Hivyo maafa yanakuwa makubwa maeneo yetu haya kutokana na nyumba zetu kutokuwa imara.

 Hivyo ni lazima sasa wananchi wetu tuwasaidie kujenga nyumba imara zinazohimili upepo mkali na mvua zenye dhuruba hali inayoonekana kuwa ikijirudiarudia.


Kwa mara nyingine natoa pole sana kwa wote na kuwaomba wadau wote wasaidie kwa kadiri watavyoweza.


Misaada yote ipelekwe kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala au Mkuu wa Wilaya ya Kahama.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog