Monday, February 24, 2014

victor_d832d.png
HATIMAYE rais Victor Yanukovych wa nchini Ukraine amekimbia mji wa Kiev baada ya bunge la nchi hiyo kupitisha kura ya kumwondoa madarakani rais huyo kutokana na shinikizo la waandamanaji.
Aidha, aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Bw. Yulia Tymoshenko ameachiwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miaka miwili jela wakati wa utawala wa Rais Yanukovych ambaye ni hasimu mkubwa wa rais huyo.
Kwa mujibu wa BBC, Naibu wa kikosi cha ulinzi wa mipaka wa taifa hilo amenukuliwa akisema kuwa ndege ya kukodiwa iliyokuwa imemchukua rais Yanukovych imenyimwa ruhusa ya kuondoka kutoka uwanja wa Donetsk, mji ambao uko mashariki mwa Ukraine ambao ni ngome ya wafuasi wake.
Akizungumza katika runinga moja ya mji wa Kharkiv, rais Yanukovych ameeleza kuwa vitendo vinavyofanyika dhidi ya serikali yake ni vya mapinduzi.
Hata hivyo, Magavana wa majimbo ya mashariki mwa Ukraine wamefanya mkutano katika mji wa Kharkiv, na kuhudhuriwa na maafisa wa Urusi kuzungumzia udhibiti haramu wa mji mkuu wa Kiev.
Wakati huohuo, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ukraine, Yulia Tymoshenko ameachiwa huru na kupokelewa kwa hisia tofauti baada ya kuwahutubia maelfu ya waandamanaji waliokusanyika katikati ya mji mkuu wa Kiev.
Akiwa ameketi katika kiti cha magurudumu, amewaambia waandamanaji kwamba wanasiasa nchini humo hawana thamani ya 'tone la damu yao' iliyomwagika wakati wa maandamano hayo.
Hata hivyo, hali katika mji wa Kiev imekuwa ya utulivu jana asubuhi siku moja baada ya kushuhudiwa mabadiliko makubwa katika mgogoro wa kisiasa wa taifa hilo.(E.L)

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog