Dar es Salaam. Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru Mkurugenzi wa zamani wa Utawala
na Utumishi (DPA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba kutokana
na upelelezi uliofanywa kuwa mbovu na wakili aliyekuwa akiiendesha kesi
hiyo kuwa mzembe.
Liyumba alikuwa akikabiliwa na kesi ya kukutwa na simu akiwa gerezani
Ukonga, Dar es Salaam, wakati akitumikia kifungo cha miaka miwili,
kilichotokana na kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi ya
Umma.
Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando alisema mahakama inamwachia huru Liyumba
kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka lililokuwa
likimkabili pasipo kuacha shaka.
Alisema wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, shahidi wa upande wa
mashtaka ambaye ni Ofisa Magereza, Patrick alidai kuwa simu aina ya
Nokia 1280 ilikutwa mikononi mwa Liyumba wakati akiwa gerezani, huku
Liyumba akidai kwenye utetezi wake kuwa siku hiyo alikwenda nayo Patrick
na kujifanya alimkuta nayo.
‘Wakati huo tulitegemea angeileta simu, lakini alitoa mkebe wa
kuhifadhia miwani na kuutenda kuwa kielelezo cha ushahidi na badala ya
simu. Akaitoa kama utambulisho tu, wakati shahidi mhusika Patrick
alikuwapo mahakamani na kutambua vielelezo vyote alivyodaiwa kukutwa
navyo Liyumba siku ya tukio.
Alisema hata huo utambulisho wa simu uliochukuliwa na mahakama,
ulichukuliwa kimakosa kwa sababu aliyepaswa kuomba kufanya hivyo
alipaswa kuwa shahidi na siyo Wakili wa Serikali kama alivyofanya
Kaganda.
Kwa upande wa mchunguzi wa kesi hiyo, Hakimu Mmbando alisema alipaswa
kubainisha ile laini ya simu yenye namba 0653 004662 ilikuwa ni ya nani
kati ya mshtakiwa na shahidi kwa sababu kulikuwa na utata.
“Kuna uwezekano ni kuwa ni kweli Liyumba alikutwa na simu gerezani,
lakini kutokana na upelelezi mbovu wa kufuatilia namba iliyotumiwa
ilikuwa ni ya nani, mazingira ya kuingizwa gerezani inaonesha wazi kuwa
mchunguzi alikuwa mzembe na uchunguzi mbovu.” Alisema Hakimu Mmbando.
0 maoni:
Post a Comment