Friday, October 11, 2013

 
*Asema uamuzi wake haukushirikisha wizara nyingine
*Adai wadau walipaswa kupewa muda zaidi, aonya rushwa


WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amemuonya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kwa mara nyingine tena kuacha tabia ya kufanya uamuzi wa jambo lolote bila kushirikisha pande zinazohusika.

Mbali ya karipio hilo, Waziri Mkuu amewataka viongozi wengine wa Serikali, kuepuka mfumo usio shirikishi katika uamuzi wao kwa kuwa unasababisha migogoro ndani ya jamii na usumbufu kwa Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu ya mgomo wa wasafirishaji wa mizigo na abiria ulioanza Oktoba 5, mwaka huu, Pinda alisema Serikali imeamua kurejesha kwa muda wa mwezi mmoja asilimia tano ya uzito wa mizigo uliozidi kwenye mizani.


Alisema hatua zilizochukuliwa na Dk. Magufuli kufuta vifungu vilivyokuwa vikiruhusu asilimia tano zilifuata sheria, lakini tatizo lililojitokeza ni kutoshirikisha pande zinazohusika ili kushauriana na kupata uamuzi wa pamoja.

Alisema mbali ya kutoshirikisha pande hizo, uamuzi wa Dk. Magufuli ulikuwa wa ghafla kwa wasafirishaji kitendo ambacho kimewapa wakati mgumu wa utekelezaji, kwa sababu wafanyabiashara walikuwa wameingia mikataba na wateja wao.

Chimbuko la mgogoro huu, ni tangazo la Dk. Magufuli alilotoa Oktoba mosi, mwaka huu la kuondoa ofa ya asilimia ya uzito uliozidi, baada ya uamuzi huo wadau wa usafirishaji wa malori na mabasi waliingia kwenye mgomo na kulalamikia hatua hiyo.

“Kutokana na mgogoro huu, nililazimika kukutana na Dk. Magufuli, baadhi ya mawaziri wa wizara zenye uhusiano na masuala haya, wanasheria na wataalamu wa masuala ya usafiri na uchumi.

Kilichoongeza mgogoro ni tafsiri ya vifungu vya sheria na kwenye kanuni ya 7 (2) na 7(3) ambacho kinaeleza wasafirishaji wa magari yenye uzito uliozidi, lakini upo ndani ya asilimia tano ya uzito unaokubaliwa kisheria, wanatakiwa kupunguza mzigo, kupinga na iwapo watashindwa kutekeleza, watatakiwa kulipia mara nne ya tozo za kawaida.

Sasa suala la asilimia tano, lilitokana na ombi la wadau wa usafirishaji kwa aliyekuwa waziri wa Ujenzi miaka ya nyuma na halikuwa sheria kamili, ndio maana limeondolewa baada ya kuonekana linatumiwa vibaya.

Nakubaliana na Dk. Magufuli, wapo baadhi ya wasafirishaji ni wakorofi na hawataki kufuata sheria…ndio maana walifanya mazoea ingawa wapo wengine wazuri na hao nawapongeza sana kutii sheria.

Maagizo
Pinda aliagiza kuanzia jana, wasafirishaji wa malori na mabasi waanze kutumia utaratibu uliokuwa ukitumika awali, huku akitoa onyo kwa atakayebainika kuzidisha uzito zaidi ya asilimia tano ya ofa anapaswa kupigwa faini.

Pia aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi, ipange utaratibu wa kupima mabasi katika mizani tofauti kati ya Kibaha na Mikese, ili kuondoa msongamano utakaokuwapo kwa siku mbili au tatu.

Alisema ofa hiyo itadumu kwa mwezi mmoja, wakati kamati itakayoundwa kwa kushirikisha wadau wote, itatafuta suluhisho la namna ya kuweka sheria hiyo vizuri ili kupata uamuzi wa pamoja.

Aliagiza mizani yote kugaguliwa ili kujua kama inafanya udanganyifu na watumishi wa mizani hiyo kwa lengo la kujipatia rushwa.

Aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kwenda na lori la mizigo kwenye mizani kupima, ili kujihakikisha kama kompyuta hizo hazijachezewa kwa lengo la kuleta usumbufu.

Alisema kamati hiyo, itahusisha watu watano kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Viwanda na Biashara, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), pamoja na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Ofisi ya Waziri Mkuu na wataalamu wengine.

Alisema kamati hiyo, inapaswa kuja na majibu ya mabasi ya abiria kama yanastahili kupimwa kwenye mizani au la, kuangalia tozo ya asilimia tano katika uzito unaozidi kuondolewa au kubakia na masuala mengine muhimu yanayohusu Jumuiya ya Afrika Mashariki juu ya usafirishaji wa abiria na mizigo.

Hata hivyo, alisema suala hilo linapaswa kufanyiwa kazi kwa makini, kwa sababu linatishia usalama wa uchumi wa nchi na kipato cha mwananchi mmoja mmoja.

Alisema licha ya baadhi ya watumishi wa mizani waliokuwa wakijihusisha na rushwa kuondolewa kwenye vituo hivyo kwa asilimia 85 sawa na wafanyakazi 400, bado rushwa inaendelea kuwapo.

Aliagiza wizara na taasisi zinazohusika kulifanyia kazi suala la rushwa katika mizani za kupimia uzito, ili kuondoa sababu zisizo na msingi.

Mgomo wa mabasi na malori ulianza Oktoba 5, mwaka huu nchi nzima ikiwa ni siku nne baada ya Dk. Magufuli kutangaza rasmi kuondoa ofa ya asilimia tano ya uzito uliozidi, jambo ambalo lilisababisha mgogoro mkubwa.

WAFANYABIASHARA
Juzi wamiliki wa malori walizungumza na waandishi wa habari na kusema hawakubaliani na uamuzi uliochukuliwa na Dk. Magufuli.

Mmoja wa wamiliki hao, ni Davis Mosha kutoka Kampuni ya Delina Group, alisema wao kama wafanyabiashara hawajagoma bali wamepaki malori yao wasiharibu barabara. Aliongeza kuwa wao ni wadau wakubwa wa kulinda miundombinu ya barabara na wanachotaka ni sheria kufuatwa.

Naye Ibrahimu Ismail kutoka Kampuni ya Usangu, alisema wamepata usumbufu mkubwa kutokana na mizani kutokuwa na viwango vilivyo sawa.

Kwa upande wake, Faisal Edha kutoka Kampuni ya Overland Logistic, alisema asilimia tano haipo Tanzania pekee, bali ipo katika nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog