WATANZANIA watakiwa
kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika Kukuza Uchumi kwa kujiunga
pamoja na kuanzisha Viwanda vidogo vidogo na vya kati.
Rai hiyo imetolewa
leo na Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi. Zainab Abdallah alipokuwa akifanya
mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii kuhusu maadhimisho ya miaka 55 ya
Uhuru wa Tanzania.
Akizungumzia kauli
mbiu ya maadhimisho hayo amesema kuwa inasadifu kile ambacho Serikali
imedhamiria kukifanya matharani suala zima la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya
viwanda kitu ambacho kimeanza kutekelezwa.
“Watanzania wanapaswa
kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kutekeleza uanzishwaji wa Viwanda vidogo vidogo
na vya kati kwani kufanya hivyo kutapunguza ama kuondoa kabisa tatizo la ajira
kwa vijana,” alisema Bi. Zainab.
Aliongeza watanzania wanapaswa
kushirikiana kwa pamoja katika kuijenga Tanzania ya Viwanda ili kuongeza
uzalishaji wa bidhaa za ndani na kuongeza fursa ya ajira kwani viwanda ni eneo
linalotoa ajira nyingi kwa wakati mmoja.
Aidha Mkuu huyo wa
Wilaya amempongeza Rais Magufuli kwa hatua kadha alizokwishachukua katika
kuhakikisha anaweka mazingira rafiki kwa wawekezaji katika sekta ya viwanda
akitolea mfano wa hatua ya Kampuni ya Bakhresa kupewa eneo la ekari elfu kumi
kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kusindika matunda.
Desemba 9 kila mwaka
Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku ya Uhuru wa Tanzania Bara ambapo kwa mwaka
huu kitaifa yatafanyika Dar es salaam na kauli ya mwaka huu ni “Tuunge Mkono Jitihada za Kupinga Rushwa na
Ufisadi na Kuhimarisha Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Nchi Yetu.”
0 maoni:
Post a Comment