Sunday, October 11, 2015


Sunderland imemteua Sam Allardyce kuwa Meneja wao mpya kwa Mkataba wa Miaka Miwili.
Sunderland wamekuwa hawana Meneja tangu Jumapili iliyopita baada ya Dick Advocaat kutimka akiiacha Klabu hiyo ikiwa Nafasi ya Pili toka mkiani mwa Ligi Kuu England.
Advocaat, Raia wa Holland mwenye Miaka 68, aliteuliwa kushika wadhifa wa Umeneja wa Sunderland Mwezi Machi wakati Timu ikiwa hatarini kushuka Daraja Msimu uliopita.
Baada ya kuinusuru kutoshuka Daraja, Advocaat alikuwa ndio amemaliza Mkataba wake lakini akaongeza Mkataba wa Mwaka mmoja ambao ungembakisha hadi mwishoni mwa Msimu huu wa 2015/16.
Katika Kipindi cha Miaka Minne, Sunderland wameajiri Mameneja 6.

Mameneja waliopita katika kipindi hicho ni Steve Bruce, alietimuliwa Novemba 2011, Martin O'Neill, Paolo di Canio, Gus Poyet, Advocaat na sasa Sam Allardyce.
Allardyce, mwenye Miaka 60 na maarufu kama Big Sam, amekuwa hana kazi tangu mwishoni mwa Msimu uliopita baada ya Mkataba wake na West Ham kumalizika.
Mara baada kutua Sunderland, Allardyce alikiri ana kazi ngumu kwa kusema: “Ni wazi ni kazi yenye changamoto kubwa. Lakini nategemea kuirekebisha Timu na kuleta mafanikio anayotaka kila Mtu.”
Big Sam ashawahi kuichezea Sunderland kati ya Mwaka 1980 na 1981 na sasa ameweka Historia ya kuwa Mtu wa Kwanza kuwahi kuwa Meneja wa Klabu mbili zenye upinzani wa Jadi, Sunderland na Newcastle.
Mechi ya kwanza kwa Allardyce kama Meneja wa Sunderland ni Ugenini na West Bromwich Albion hapo Oktoba 17 na ya kwanza Uwanja wa Nyumbani Stadium of Light ni hapo Oktoba 25 dhidi ya Newcastle.


Sam Allardyce:Kazi ya Umeneja
1989–1991 West Bromwich Albion (Msaidizi)
1991–1992 Limerick (Meneja Mchezaji)
1992 Preston North End (Meneja wa Muda)
1994–1996 Blackpool
1997–1999 Notts County
1999–2007 Bolton Wanderers
2007–2008 Newcastle United
2008–2010 Blackburn Rovers
2011–2015 West Ham United
2015– Sunderland

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog