Thursday, September 10, 2015


SIMBA SC inafunga safari leo kutoka Zanzibar kwenda Tanga tayari kwa mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi dhidi ya wenyeji wao, African Sports. Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema baada ya maandalizi ya tangu Julai, anaamini kabisa kikosi sasa kipo tayari kwa Ligi Kuu. “Mwalimu alipatiwa kila alichohitaji katika maandalizi. Ushauri wake ulifuatwa katika uundwaji wa timu na matayarisho kwa ujumla. Kambi ya aina gani, wakati gani kila alipohitaji alipata. Mechi za aina gani za majaribio na wakati gani, kila alipohitaji alipata, na kila mchezaji aliyesajiliwa alipitia mikononi mwake kwanza akamuangalia na kumuidhinisha. Nadhani upande wetu kama viongozi, tumecheza vizuri katika eneo letu,”amesema Poppe.
Basi la Simba SC litawapokea wachezaji wa SImba SC bandarini Dar es Salaam kuwapeleka Tanga tayari kwa mechi na African Sports Jumamosi
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema anaamini kabisa sasa ni wakati wa benchi la Ufundi na wachezaji nao kufanya kazi yao ili kuwapa raha wana Simba SC. “Ushindi tu hadi ubingwa, hiyo ndiyo kiu ya wana Simba wote na ndiyo maana tumetumia gharama kubwa ya kuiandaa timu, kuanzia kambi ya Lushoto na baadaye Zanzibr kwa miezi miwili,”amesema.   Msimu mpya wa Ligi Kuu unaanza Jumamosi, na mbali na Smba SC na African Sports Mkwakwani,  Ndanda FC watakuwa wenyeji wa Mgambo Shooting Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, Majimaji FC wataikaribisha na JKT Ruvu Uwanja wa Majimaji, Songea na Azam FC wataikaribisha Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Stand United watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Toto Africans wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa Kambarage Shinyanga na Mbeya City watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine, wakati Jumapili mabngwa watetezi Yanga SC wataanzia nyumbani na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Simba SC inaingia katika msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara chini ya kocha mpya, Muingereza Dylan Kerr aliyeanza kazi mapema Julai, baada ya kuachana na Mserbia, Goran Kopunovic aliyetaka dau kubwa ili kuongeza Mkataba.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog