CHELSEA iliyokuwa inayumba katika Ligi Kuu
England ambayo wao ni mabingwa watetezi, imeibuka na kuitwanga Arsenal kwa
mabao 2-0.
Ushindi wa Chelsea huenda haukupewa nafasi kubwa
kutokana na timu hiyo kuanza ligi kwa kusuasua, huku kocha wake, Jose Mourinho
akionekana kutojielewa.
Lakini sasa imeibuka na kushinda dhidi ya Arsenal
iliyoonekana kubadilika na angalau kuanza kushinda dhidi ya Chelsea baada ya
ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya vigogo hao wa Stamford Bridge kwenye mechi ya
Ngao ya Jamii.
Ajabu, wakati Chelsea inaibuka na ushindi, juzi,
haujawa gumzo, badala yake kila mmoja anazungumzia kuhusiana na mshambuliaji wa
Chelsea, Diego Costa.
Kwamba raia huyo wa Hispania mwenye asili ya
Brazil, alikuwa tatizo na alipaswa kupewa kadi nyekundu. Gumzo kwamba
alisababisha beki Gabriel alambwe kadi nyekundu kwa kuwa aliparura shingoni,
alimsukuma, pia alifanya ubabe kwa beki mwingine wa Arsenal, Laurent Koscielny.
Katika purukushani hizo, Costa aliambulia kadi ya
njano lakini Kocha Arsene Wenger amesema mshambuliaji huyo alistahili kadi
nyekundu kabisa, huku akiamini mwamuzi Mike Dean na wasaidizi wake hawakuwa
makini sana ingawa alikataa zaidi kuzungumzia kuhusu waamuzi.
Kinachoweza kushangaza zaidi ni kwamba pamoja na
kelele zote, Costa hakupatikana na faulo hata moja ukiachana na ile kadi.
Hakuonekana kucheza madhambi au vinginevyo ingawa kweli purukushani zake
ziliwavuruga kabisa Arsenal, wakashindwa kufikia malengo yao kiuchezaji.
Nani kasahau ‘footbal is a game of contact’.
Mtacheza vipi soka bila ya kugusana, angalau kusukumana au kuangushana?
Mourinho alitolea mfano wa mchezo wa ‘badminton’, kwamba watu hawagusani na
soka haiko hivyo. Sawa na hapa ungeweza kutolewa mfano wa draft!
Utajiuliza hivi; hawa Arsenal walikuwa wanakutana
kwa mara ya kwanza na Costa? Jibu, hapana, sasa vipi iwe ndiyo ishu wakati kuna
kadi nyekundu nyingine ya Santi Cazorla ambayo iliwavuruga kabisa.
Arsenal ni timu yenye mashabiki walalamishi
kuliko wote duniani. Kama siyo, sasa vipi wanalialia, kwani hawakujipanga? Au
waliingia uwanjani wakiwa hawajui wamejipangaje kukabiliana na jogo feio?
Jina jogo feio kwa Lugha ya Kireno ni mchezaji
mwenye mchezo wa vurugu, huo ni uchezaji wa Costa akiwa Hispania, jina ambalo
linatambulika sana.
Kuna ‘game plan’, yaani mipango ya mchezo.
Arsenal lazima walijua Costa ndiyo atakuwa tatizo na atatumika kuwachanganya
mabeki. Sasa vipi walikubali kuchanganywa kweli na kutoa nafasi Mhispania huyo
auchukue mchezo wote?
Costa ndiye aliyeipa Chelsea ushindi kwa kuwa
ameonekana kuwa ‘profesheno’ zaidi ya wanavyomsema. Kwa sababu hizi tatu.
Moja:
Straika anatakiwa kuisaidia timu yake kupata
ushindi kwa mambo matatu. Kufunga, kutoa pasi ya bao au kusaidia kuwavuruga
mabeki wa timu pinzani.
Yeye amefanikiwa kuwavuruga mabeki na kikosi
kizima cha Arsenal, amepunguza mtu baada ya beki kutolewa.
Mbili:
Amewatoa Arsenal mchezoni, wamepaniki na
kushindwa kucheza walivyotakiwa au kama walivyoanza kipindi cha kwanza:
Tatu:
Wenger pia alionekana kuingia kwenye mtego wa
Costa. Badala ya kuendeleza mipango, akatumia muda mwingi kulalamika dhidi ya
jogo feio akimuacha Mourinho akiendeleza mipango ya kummaliza.
Sasa kwa Costa anataka nini zaidi? Kwa mashabiki
na uongozi wa Chelsea anastahili pongezi kwa kazi nzuri.
Ukiangalia hakumuumiza mtu, lakini amevuruga
mbinu za wapinzani. Pia amekuwa akicheza hivyo na mifano utaona alipozozana
nusura azichape na Steven Gerrard pale Chelsea walipokutana na Liverpool, msimu
uliopita.
Unakumbuka vita yake na beki Martin Skrtel wa
Livepool au John O’shea wa Sunderland? Najua bado hujasahau vita yake na David
Luiz wa PSG na vurugu nyingine kibao.
Siku moja Costa hatakuwa shujaa, kwa kuwa anaweza
akakosea hesabu na kusababisha alambwe kadi nyekundu kwa kuwa kwa kipindi hiki
waamuzi watamtupia jicho kwa karibu kukwepa lawama anazosukumiwa Dean na
wasaidizi wake.
Ukweli ni kwamba sasa Costa ni shujaa wa Chelsea,
hasa kwa mechi ya juzi na kama alivyosema Mourinho, kwamba alivyocheza Costa
ilikuwa sahihi na ndiyo mipango hasa ya mchezo ilivyotakiwa iwe. Hivyo Arsenal,
waache kulialia.
0 maoni:
Post a Comment