Wachezaji
wa Yanga SC wakisherehekea na Ngao ya Jamii wiki iliyopita baada ya
kuifunga Azam FC kwa penalti 8-7 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
YANGA
SC wanatarajiwa kuweka kambi ya wiki moja visiwani Zanzibar kuanzia
Septemba 6, kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itakayoanza
wiki itakayofuatia.
Katibu
Mkuu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha amesema kwamba kwa sasa kikosi
kipo Dar es Salaam kikiendelea na mazoezi chini ya kocha Hans van der
Pluijm.
“Mazoezi
yanaendelea Dar es Salaam kwa sasa, kama unavyojua, wachezaji wetu
wengi wamekwenda kuzitumikia timu zao za taifa, hivyo waliobaki
wanaendelea na mazoezi,”amesema Dk. Tiboroha.
Mabingwa
hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, watafungua dimba na Coastal
Union ya Tanga Septemba 13 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wiki
iliyopita, Yanga SC ilifungua pazia la Ligi Kuu kwa ushindi wa penalti
8-7 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Siku hiyo, kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ alipangua penalti mbili za
beki raia wa Ivory Coast, Serge Wawa Pascal na mshambuliaji Ame Ali
‘Zungu’, wakati kipa wa Azam FC, Aishi Manula naye alicheza penalti ya
Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’.
Penalti
za Yanga SC zilifungwa na Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Amissi Tambwe,
Andrey Coutinho, Godfrey Mwashiuya, Thabani Kamusoko, Mbuyu Twite na
Kelvin Yondan aliyepiga ya mwisho.
Penalti
za Azam FC zilifungwa na Kipre Herman Tchetche, Nahodha John Raphael
Bocco, Himid Mao Mkami, Aggrey Morris, Jean Baptiste Mugiraneza, Erasto
Nyoni na Shomary Kapombe.
Ushindi
huo ni sawa na kisasi baada ya Yanga SC kufungwa kwa penalti 5-3 katika
Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame
Julai 29, mwaka huu Uwanja wa Taifa, baada ya sare ya 0-0.
Ni
mara ya tano sasa Yanga SC kutwaa Ngao ya Jamii ikiwa ni rekodi, baada
ya kuifunga Simba SC mara mbili, mwaka 2001 mabao 2-1 na 2010 kwa
penalti 3-1 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika ya 90, kabla ya
kuifunga Azam FC miaka mitatu mfululizo, 2013 bao 1-0 na 2014 mabao 3-0.
Inafuatia
Simba SC iliyotwaa Ngao mara mbili, mwaka 2011 wakiifunga Yanga SC 2-0
na 2012 wakiifunga Azam FC 3-2, wakati Mtibwa Sugar ni timu nyingine
iliyowahi kutwaa Ngao mwaka 2009 ikiifunga 1-0 Yanga SC.
0 maoni:
Post a Comment