Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro, Charles Mkwasa amesema vijana wake wapo tayari kuwavaa Nigeria Septemba 05, 2015 katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za AFCON mwaka 2017.
Mkwasa ambaye yupo nchini Uturuki na kikosi cha timu ya Taifa kambini kwa mazoezi ya takriban wiki moja, amesema vijana wameonyesha mabadiliko makubwa baada ya kupata wiki moja ya mazoezi ya pamoja.
“Mazoezi wanayofanya hapa yamewajenga stamina, unaweza kuona wanacheza kwa nguvu muda wote, wanakaba na kushambulia kwa pamoja, hii ni dalili nzuri ya vijana kuelekea katika mchezo huo dhidi ya Nigeria”amesema Mkwasa.
Kocha huyo wa timu ya Taifa amesema timu yake imefanya mazoezi katika nyanja zote ikiwemo mazoezi ya kujenga mwili na kucheza mpira wa kasi.
Aidha Mkwasa amesema kambi hiyo imekua na faida kubwa sana kiufundi, kufuatia kupata nafasi ya kukaa sehemu tulivu na wachezaji kuwapa mazoezi ambayo waliyapanga katika program hiyo ya kambi nchini Uturuki.
Taifa Stars imeendelea na mazoezi leo asubuhi, na inatarajiwa kufanya mazoezi yake ya mwisho kesho siku ya jumatau, kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani Tanzania kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo huo.
0 maoni:
Post a Comment