………………………………..
MABINGWA wa soka wa Tanzania
Bara, Yanga, Juni 27, mwaka huu wanatarajia kuvaana na SC Villa ya
Uganda katika mchezo wa kirafiki utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, ukiwa na lengo la kukusanya fedha za kujengea kituo cha watoto
wanaoishi kwenye mazingira magumu na walemavu wa ngozi, yaani albino.
Akizungumza Dar es Salaam jana
katika ukumbi wa makao makuu ya Yanga yaliyopo Jangwani, jijini, Katibu
Mkuu wa klabu hiyo, Jonas Tiboroha, alisema kuwa katika mchezo huo
watachezesha kikosi chao kamili, kikiwajumuisha wachezaji wapya na nyota
wa zamani.
Alisema wameamua kushiriki
katika tamasha hilo kama sehemu ya kuonyesha jinsi wanavyoguswa na
jamii, ikiwa ni baada ya kuombwa kufanya hivyo na Taasisi ya Nyumbani
Kwanza Media kwani hata klabu kubwa Ulaya zimekuwa zikiafnya hivyo.
“Baada ya kuletewa wazo hili na
wenzetu wa Nyumbani Kwanza, tulikubaliana nao kwani ni zuri. Tumeona
klabu ya Yanga isipate isipate sifa kwa kutwaa ubingwa tu, bali pia hata
kufanya shughuli za kijamii kama hizi. Uongozi umebariki na hata Kocha
Mkuu na benchi lote la ufundi lina taarifa na ndio maana tumeanza
mazoezi mapema zaidi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa Nyumbani Kwanza Media, Mossy Magere, alisema kuwa wazo la
kuandaa tamasha hilo lilikuja baada ya kutafakari ni vipi wanaweza
kusaidia makundi yenye mahitaji maalumu na wakaona ni vema kuishirikisha
Yanga wakiwa kama mabingwa wa Tanzania Bara.
“Mapato yatakayopatikana
yatafanya shughuli kusudiwa kwa kuanza rasmi ujenzi wa kituo huko
Bagamoyo, mkoani Pwani na tutakuwa tukifahamishana kila hatua ya mradi
huo utakaogharimu Sh bilioni 1.5 ambao tumepania uwe mfano wa kuigwa na
wengine,” alisema Mossy.
Aliwapongeza Yanga kwanza kwa
kutwaa ubingwa wa Bara, lakini pia kukubali kushirikiana nao katika
kufanikisha tamasha hilo la aina yake.
Awali mechi hiyo ilikuwa ichezwe
kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, lakini kutokana na ushauri wa
Tiboroha, waliamua iwe Dar es Salaam ili kupunguza gharama za maandalizi
yake, hasa katika suala zima la usafiri kwa timu na mengineyo.
0 maoni:
Post a Comment