Taifa stars iliwasili uwanjani hapo saa 3:30 asubuhi na kukuta mashabiki wakiangalia mazoezi ya Yanga ambayo inajiandaa na mashindano ya Kagame yanayotarajia kuanza Julai, 9.
Baada ya kuwasili meneja wa timu hiyo Boniface Clemence alianza kushusha vifaa vya mazoezi na wachezaji kuanza kushuka, mashabiki walipowaona ndipo wakaanza kupiga kelele za kuzomea huku wengine wakiwaita watalii hali iliyofanya kocha kuamuru vifaa virudishwe ndani ya gari.
“Buuuh watalii hao, buuu watalii hao,” walizomea mashabiki hao.
Kelele hizo ziliongezeka kwani mashabiki waliokuwa kwenye jengo la Machinga nao walipowaona walizomea zaidi.
Baadae zomeazomea hiyo ilikuja kutulizwa na meneja Clemence pamoja msaidizi wa rais wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi Juma Matandika waliowataka mashabiki kuwa wazalendo kwani hiyo ni timu yao ya taifa hakuna haja kuizomea.
“Jamani mnapozomea haisadii kwani hii ni timu yetu sote watanzania ni kweli tumefungwa lakini angalia rekodi ya Misri, hakuna timu ambayo imekwenda kucheza pale ikatoka bila kufungwa tena kwa idadi kubwa ya mabao,”, alisikika akisema Clemence.
Baada ya hali kuwa shwari wachezaji na benchi la ufundi walitoka wakaingia Uwanjani kuanza mazoezi huku wakipishana na Yanga ambao nao walikuwepo kwenye Uwanja wa Karume wakifanya mazoezi.
Taifa stars inatarajiwa kuondoka leo kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya mchezo dhidi ya Uganda utakaochezwa keshokutwa.
0 maoni:
Post a Comment