Baadhi
ya Wanamichezo wa Polisi walioshiriki Michezo ya Wakuu wa Majeshi ya
Polisi kusini mwa Afrika mwaka 2013 nchini Namibia wakiwa katika picha.
Timu za Jeshi la Polisi Tanzania
zitakazoshiriki michezo ya Umoja wa Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa nchi
za kusini mwa Afrika (SARPCCO), mwishoni mwa mwezi julai nchini
Swaziland zinaendelea kujifua vyema katika kambi yao inayoendelea
katika chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA).
Akizungumza na blog hii Mkuu wa
kitengo cha michezo cha Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi
SSP Jonas Mahanga alizitaja timu zilizopo kambini kuwa ni pamoja na
Timu ya Mpira wa miguu, pete, riadha na vishale ambapo hivi sasa
zinajifua kuhakikisha kuwa zinakuwa vizuri pindi michuano hiyo
itakapoanza kutimua vumbi.
Amesema timu hizo zitaanza
kucheza michezo ya kirafiki ili kujipima nguvu na kuhakikisha wanafanya
vizuri kwa kuwa michezo ya mwaka huu itakuwa na ushindani mkubwa
kutokana na nchi zilizothibitisha kushiriki kujipanga vizuri.
SSP Mahanga amesema mpaka sasa
nchi kumi na nne zimeshathibitisha kushiriki michuano hiyo na
wanaendelea kuwakaribisha wadhamini mbalimbali watakaoweza kusaidia
safari hiyo ili kuliletea taifa sifa.
Aidha amesema wachezaji wengi wa
riaha wanaendelea na mazoezi katika timu ya taifa ya riadha na wengine
wapo nchini Kenya ambapo muda utakapowadia wataungana na wenzao katika
kambi hiyo ya Dar es Salaam.
Kwa upande wake kocha wa timu
ya mpira wa miguu Corporal John Tamba amesema wachezaji wake wamekuwa
wakionyesha kiwango kizuri katika mazoezi kwa kuwa wengi wao wametoka
katika mashindano hivi karibuni.
Amesema wachezaji
wengi waliopo kambini wanatoka katika timu za Polisi Morogoro, Dodoma,
Dar es Salaam, Tabora na Mara ambapo alisema kupitia michezo ya kirafiki
atahakikisha timu yake inakuja na ushindi.
0 maoni:
Post a Comment