Kagera Sugar imeshinda mechi tano Uwanja wa Kambarage tangu ihamishie maskani yake mjini Shinyanga ikitokea Mwanza ilikopoteza mechi tatu mfululizo na kulazimika kuhama.’ KAGERA Sugar FC imesahihisha makosa ya kufungwa 2-1 dhidi ya Simba SC wiki iliyopita baada ya kuilaza Ruvu Shooting Stars mabao 2-0 katika mechi pekee ya leo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Kwa matokeo hayo, Kagera Sugar FC inayonolewa na Mganda Jackson Mayanja, imeendelea kubaki nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikifikisha pointi 31 baada ya mechi 22, pointi nne nyuma ya Simba SC inayokamata nafasi ya tatu baada ya mechi 21.
Kikosi cha Mkenya Tom Olaba cha Ruvu Shooting Stars kimeendelea kubaki nafasi ya nane katika msimamo wa ligi kikiwa na pointi 26 baada ya mechi 22.
Victor Hangaya amefunga bao la kwanza la Kagera dakika mbili baada ya kuanza kwa kipindi cha pili kabla ya Atupele Green kuongeza la pili katika dakika ya 51 na kuihakikishia Kagera Sugar FC ushindi wa tano Uwanja wa CCM Kambarage msimu huu tangu wahamishie maskani yake mjini Shinyanga ikitokea Mwanza Januari mwaka huu.
Kagera Sugar FC imelazimika kuishi mithili ya kumbikumbi kwa kuhamaha msimu huu kutokana na ukarabati wa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, unaofandhiliwa na FIFA.
Katika mechi ya leo kikosi cha Kagera kimemkosa mshambuliaji wake tegemeo mwenye magoli 10 msimu huu, Rashid Mandawa kutokana na mchezaji bora huyo wa mwezi Novemba wa ligi hiyo kuwa na kadi tatu za njano.
0 maoni:
Post a Comment