Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Mohamed Msangi.
MSHITUKO wa matukio ya
mfululizo ya ajali, umeendelea kugubika nchi, baada ya watu 20 kupoteza
maisha katika ajali ya basi dogo aina ya Toyota Hiace, iliyotokea jana
wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
Ajali hiyo ambayo
taarifa na picha zake zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii,
imesababisha taharuki kutokana na ukaribu wake na matukio mengine ya
ajali yaliyotokea wiki hii.
Baadhi ya wakazi wa jirani na eneola tukio wakitazama gari lilivyopata ajali kando kando ya mto Kiwira.
Tangu Jumapili iliyopita
mpaka jana, siku zisizozidi sita kumetokea ajali kubwa tatu
zilizohusisha mabasi ya abiria na kuteketeza maisha ya watu 40.
Mbali na ajali hizo,
wiki hii Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani,
Mohamed Mpinga alitoa takwimu zilizosababisha huzuni kwa Watanzania,
kwamba kati ya Januari mosi na Aprili 12 sawa na siku 102, watu 969
walipoteza maisha katika ajali za barabarani.
Wananchi wa Kiwira wakiangalia baadhi ya Miili ya Watu waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo.
Ajali za wiki
Jumatano wiki hii, basi
la Air Jordan lililokuwa likitokea mkoani Mwanza kwenda Arusha, lilipata
ajali na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi 20.
Ajali hiyo ilitokea
wakati Watanzania wakiwa na kumbukumbu ya ajali iliyotokea Jumapili ya
wiki jana, ambapo watu 19 waliteketea kwa moto, baada ya basi la Kampuni
ya Nganga Express na lori aina ya Fuso kugongana uso kwa uso na kuwaka
moto katika eneo la Iyovi, Milima ya Udzungwa, mkoani Morogoro.
Ajali ya Mbeya
Akizungumza na gazeti
hili jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Mohamed Msangi, alisema
ajali hiyo mpya imetokea katika eneo la Ilongo ambalo limebatizwa jina
la Uwanja wa Ndege karibu na Kiwira, ambapo watu 18 walipoteza maisha
papo hapo.
“Watu wanne
waliojeruhiwa, mmoja alikuwa katika hali mbaya na kwa bahati mbaya
alifia njiani wakati akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe kwa
matibabu,” alisema Kamanda Msangi.
Kamanda Msangi alisema
chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na dereva kutokuwa makini katika
uendeshaji wake. Taarifa zilizotufikia baadae, zilieleza kuwa abiria
mwingine aliyekuwa akipatiwa matibabu, alifariki akiwa hospitalini.
Mashuhuda
Mashuhuda wa ajali hiyo
walidai kuwa chanzo cha ajali ni mwendokasi uliosababisha dereva
ashindwe kumudu gari hilo katika mteremko wenye kona, akajikuta gari
likimshinda na kutumbukia katika Mto Kiwira.
Walidai kuna uwezekano
dereva huyo alikuwa akikimbizwa na baadhi ya madereva wa mabasi aina ya
Toyota Coaster, yanayofanya safari zake kati ya Mbeya, Tukuyu na Kyela.
0 maoni:
Post a Comment