Tuesday, March 4, 2014


Katika maisha yangu sijawahi kuona watu wenye imani kali kama wahubiri dini. Mapadri, masheikh, wachungaji hawa watu wana imani kali sana na dini zao. Imani zao zimejengwa kwa kusikia mafundisho ya vitabu vitakatifu. Hata biblia imenena kuwa "imani huja kwa kusikia, tena kwa kusikia neno la Mungu."
Ili shekh uitwe shekh lazima uwe una imani thabiti ya dini ya kiislamu iliojengwa kwa misingi ya Q'urani. Na mchungaji vivyo hivyo, lazima awe amejazwa neno la Imani kupitia misingi thabiti ya biblia. Lakini hakuna Sheikh aliyekua Sheikh bila kupitia mafundisho thabiti ya dini ya kiislam, na ili uwe padre lazima upitie seminari.
Achana na seminari za siku hizi, kila mtu akijenga shule anaiita seminari. Matokeo yake wanatuzalishia magigisi na magobo. Seminari zilikua zamani bwana, mtu akitoka seminari hata bila kukwambia utamjua tu. Tabia hata hekima yake itaongea tu. Wachungaji na Mapadre waliosoma seminari za kale walifundwa wakafundika, walikanywa wakakanyika.vHawa watu ni ngumu kuwatenganisha mbali na imani yao, hawa watu huwezi kuwabadilisha kwenye kile wanachokiamini. Mchungaji na padre walishafundishwa, wakasikia pia wakasoma kuwa isaka ni mzaliwa wa kwanza halali wa Ibrahim, asilani huwezi kumbadilisha na kumwambia Ismail ndie mzaliwa wa kwanza halali wa Ibrahim. Kesha ukeshavyo, hubiri uhubirivyo hawezi kubadili msimamo wake asilani. Mpige mawe kama Stephano, muwekee kisu shingoni bado atachukua mbundugo na kuendelea na Imani yake. Mchungaji anaamini akimuombea kiwete atatembea tena, akimuombea kipofu ataona tena, kiziwi pia atasikia tena.
Muda mwingine kipofu huwa haamini kuwa siku moja akiombewa ataona, ila mchungaji ana imani asilimia zote kuwa kipofu lazima atapokea uponyaji. Hata akimuombea mara ya kwanza kipofu asione ila bado atakua na imani ipo siku kipofu huyo ataona tena kwakuwa alishawahi kuombea vipofu wengine wakaona tena. Huo ndo ujasiri wa mchungaji, hiyo ndio imani ya mchungaji.
October 22 1949 mjini Strasbourg alizaliwa muinjilisti wa soka. Mwenye imani kali kama Ibrahim. Huyu ni mtoto wa mzee Alphonce, aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa vipuri mjini Strasbourg. Alitumia muda mwingi kuangalia mpira akiwa bar. Hakika soka ilikua ndani ya damu yake. Alitumia mbinu alizoziona bar na kuzihamishia kwenye timu yake ya kijiji. Tangu kijana alipenda kazi ya ukocha kuliko kucheza mpira. Muda mwingi alikua akipanga kikosi kwenye timu yake ya kijiji amayo baba yake alikuwa akifundisha. Maisha yake ya soka kama mchezaji yalianzia kwenye timu ya kijiji cha Duttlenheim, kijiji ambacho alikulia mseminari huyu.
Hakuna aliyemjua muinjilisti huyu kwenye maisha yake ya uchezaji. Alitundika daruga akiwa na timu ya RC Strasbourg na kufungua ukurasa mpya katika ngazi ya ukocha. Maisha yake kama kocha yalianza mwaka 1981 mara alipohitimu shahada yake ya biashara na kukabidhiwa mikoba kama kocha wa timu ya vijana katika timu ya RC Strasbourg. Mwaka 1983 akateuliwa kuwa kocha wa vijana wa timu ya Cannes kabla ya kutimkia katika klabu ya Nancy Lorraine mwaka mmoja baadae, mwaka 1987 klabu ya Nancy ikashuka daraja.Wengi walifikiri huo ndio ungekua mwisho wa mseminari huyu katika maisha yake kama kocha. La hasha huo ndio ulikuwa mwanzo wa nyota yake kuangaza.
Mnamo mwaka 1987 klabu ya Monaco ikampa ajira ya kuwa kocha wa timu hiyo, uteuzi huo ulileta maswali mengi sana, hakuna aliyeamini klabu kubwa kama Monaco itamteua kocha aliyeishusha timu daraja."Hakika huyu ni mwana wa Mungu",ni mmoja wa watu wenye bahati katika sayari yetu.
Msimu wake wa kwanza akiwa na Monaco akaiwezesha klabu hiyo kuwa bingwa wa ligi kuu ya Ufaransa, pia mwaka 1991 aliiwezesha Monaco kuwa bingwa wa kombe la Ufaransa.
Katika kipindi chake kama kocha wa Monaco alipata kuwasajili wachezaji kama Glenn Hoddle na George Weah ambae baadhi ya watu walikejeli usajili wake lakini mwamba huo wa Afrika miaka kadhaa mbele ukaibuka kuwa mchezaji pekee bora duniani kuwahi kutokea kwenye Dunia yetu ya tatu. Huo ndio ujasiri wa mseminari huyu ulipoanzia.
Mwaka 1994 alishindwa kukubaliana na uongozi kuhusu mkataba wake na klabu ya Monaco. Kumbuka klabu ya Monaco ilimzuia kwenda kufundisha katika klabu ya Bayern Munich mwaka huo huo. Huo ndo ulikua mwisho wake wa huduma kama kocha kwa klabu ya Monaco na Ufaransa kwa ujumla. Alitimkia kwenye klabu ya Nagoya Grampus kabla ya kupigiwa pande na rafiki yake David Dein kuinoa klabu ya Arsenal mwaka 1996. Timu zote alizofundisha awali zilikua shule hapa ndipo alipoanza rasmi kazi yake ya uinjilisti.
Utamwambia nini huyu mtu akuelewe wakati washabiki wa Arsenal hawakumuelewa alipotumia pesa kumnunua Dennis Bergkamp. Wengi walilalamika pesa zilizotumiwa kumnunua mdachi huyo. Ni yeye pekee aliyeamini Begkamp ana thamani hiyo. Baadae kidogo Bergkamp akawaonesha Wenger alikua sahihi kuliko wadau na mashabiki. Unamkumbuka Anelka? Wakati anasajiliwa kinda huyu kila mtu alimnyooshea kidole. Magazeti yote yakamuadaa na kuona kama amefanya kituko cha usajili. Ila mzee huyu na imani kama ya Abrahamu akamuamini Anelka, Anelka nae akampa kocha wake kile alichokiona kutoka kwake.
Mashabiki na wadau wakabaki midomo wazi huku vyombo vya habari vikiwa vimepigwa bao la pili na mfaransa huyu. Robin van Persie aliandamwa na majeruhi, mashabiki wengi sana walipendekeza auzwe hasa pale Juve walipotuma ofa, lakini muinjilisti huyu akamkumbatia kilema wake huku akiamini ipo siku kilema wake atatembea tena. Aliamini ipo siku RVP atakua gumzo katika ligi ya Uingereza ndivyo ilivyotokea, washabiki waliotaka auzwe wakasahau wakaanza kumshangilia. Aaron Ramsey, huyu mpiganaji wa kiingereza, wenyewe humuita Rambow, ni mchezaji bora wa Arsenal mwaka 2013. Licha ya kupata majeruhi bado anatarajiwa kua mchezaji bora wa Arsenal mwaka 2014. Huyu ni muingereza haswa, hujitoa asilimia mia ndani ya uwanja, hutoa kila kitu kwa ajili ya timu yake. Kila mshabiki wa Arsenal anampenda Rambow, ila bila imani ya kocha wake huyu ramsey asingekuwa mchezaji wa Arsenal kwa sasa. Huyu mtoto wa mzee Alphonce ana imani kama ya David Oyedepo, aliamin ipo siku Ramsey atakuwa nyota. Lakini mashabiki wa Arsenal waliona Ramsey ni kama mgonjwa wa ukimwi, hawakuamini kama atapona siku moja. Ni yeye tu aliyemuamini.
Huyu mzee wetu kuna mambo matatu ameamua kuyafumbia macho. Hayo ndo yalioifanya Arsenal ikose ubingwa kwa miaka nane na huu unaenda mwaka wa tisa bado anafanya makosa yale yale yatakayomfanya atoke kapa tena.
Kosa la kwanza ni kufumbia macho nguvu ya pesa ya Chelsea na Man City. Bado anaiishi jana yake leo. Anaamini soka la karne ya 20 ni sawa na soka la karne hii. Katika utawala wake alikuwa akishindana na Manchester United pekee. Manchester United ikiteleza Arsenal ilikua haifanyi makosa. Tangu utawala wa Chelsea na Man City uanze Aresnal wametwaa taji moja tu. Arsenal ya sasa inahitaji kutumia mabavu ya pesa ili kushindana na Chelsea na Manchester City. Huwezi kuchukua kombe wakati unawategemea Sanogo na Giroud na huku mwenzako ana Dzeko na Jovetic katika benchi la wachezaji wa akiba.
Pili ni Kuendelea kukumbatia wachezaji wasiompa matokeo. Tunajua kama wewe ni baba wa imani kwenye soka ila kwanini usijifunze kwa yaliyokupata awali. Richard Wright, Denilson, Andre Santos, Francis Jeffers, Igors Stepanovs, Sebastian Squillaci hawa ni miongoni wa wachezaji mizigo aliowaamini na kuwapa nafasi. Licha ya kuwaamini na kuwang'ang'ania bado hawakumpa matokeo, mwisho wa siku wachezaji hao wakaitia hasara klabu. Ila bado hajakoma tu, bado anaamini kwa Giroud, akimuangalia Giroud anamuona Henry ndani yake. Imani yake ndio inamuongoza hivyo.
Kosa lake kubwa na la mwisho kushindwa kufanya mabadiliko na marekebisho kwa kila sekta ndani ya timu kwa msimu.
Kuna msimu arsenal inakuwa na beki nzuri na viungo wazuri lakini inakosa mmaliziaji mzuri(mfano msimu huu), kuna msimu inakuwa na beki mbovu ila wanapata viungo wazuri na washambuliaji wazuri, pia kuna msimu wanakuwa na beki imara na washambuliaji maridadi lakini viungo wanarega. Wakati akiendelea kumsubiri RVP, Cesc Fabregas alikua akiibeba timu licha ya kuongozwa na safu nyepesi ya ushambuliaji iliyokua ikiongozwa na Adebayor. Mungu si Athuman Robbin van Persie akarejea lakini msimu unaofuata tangu RVP arejee akamuuza Cesc Fabregas.
Kiungo cha Arsenal kikarega. Akaanza kumuamin Ramsey huku Thomas Rocisky akirejea taratibu kuziba pengo la Fabregas kipindi hicho RVP anaibeba timu, lakini msimu unaofuata akamuuza RVd ambaye alikua mmoja wa washambuliaji hatari Duniani na kumnunua Olivier Giroud kama mbadala wake. Mpaka wa leo Giroud viatu vya RVP havimtoshi.
Pata picha Arsenal ya leo ingekua na RVP na Samir Nasri, ungekua unahitaji nini kwenye dunia ya soka. Arsenal ilikua inahitaji mtu kama Suarez ili avae viatu vya RVP, keshokutwa atatafuta mshambuliaji mkali huku akisahau Rocisky na Cazorla umri unawatupa mkono.
Huyu kila msimu anakomaa kuimarisha sekta moja au mbili tu. Kwake siku zinaganda, miaka haiendi. Huyu ndie Baba wa imani, mimi napenda kumuita muinjilisti.
Huyu ndie ARSENE WENGER mwenye roho ya kiseminari, imani ya kichungaji, huwa hakubali kupingwa kutoka kwenye kile anachokiamini, huwa hapangi kushindwa, ila anashindwa kupanga.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog