Thursday, February 27, 2014



ronaldo_8e1ea.jpg


REAL Madrid imejihakikishia kucheza robo fainali ya michuano ya 
Ligi ya Mabingwa barani Ulaya baada ya kuitandika Schalke 04 ya Ujerumani
 mabao 6-1. Mchezaji bora wa dunia, Cristiano Ronaldo, mchezaji 
aliyevunja rekodi ya usajili ulimwenguni Gareth Bale pamoja 
na mchezaji mahiri Karim 
Benzema walihakikisha kila mmoja wao anatupia nyavuni magoli mawili ili
 kuifanya Real Madrid, vinara wa ligi kuu nchini Hispania, kuisulubu vilivyo 
Schalke 04 tena kwenda
 dimba lake la nyumbani, Veltins-Arena. Bao la kufutia machozi 
la Wajerumani hao lilifungwa
 na Klaas Jan Huntelaar katika dakika ya 90.
Alikuwa Karim Benzema katika dakika ya 13 tu alipopokea mpira kutoka kwa 
Cristiano Ronaldo na kuutumbukiza wavuni kama ishara ya ufunguzi rasmi wa 
karamu ya magoli ya miamba hao wa soka nchini Hispania. Kisha, panapo 
 dakika ya 21, mchezaji aghali zaidi aliyesajiliwa kutoka Tottenham Hotspur ya
 Uingereza, Gareth Bale akautia mpira kimiani baada ya kupokea pasi kutoka kwa 
Karim Benzema.

Mwamuzi Howard Webb, anayetajwa kuwa mwamuzi bora zaidi duniani kwa sasa 
 alipopuliza kipenga kuashiria mapumziko, Real Madrid wakarejea vyumba vya 
mapumziko wakiwa tayari na magoli mawili nunge.

Timu hizo ziliporejea dimbani kwa ngwe ya mwisho, ilimchukua Cristiano Ronaldo 
dakika saba tu kuibadili pasi kutoka kwa Gareth Bale kuwa goli la tatu. Dakika tano 
baadaye, dakika ya 57, Karim Benzem akafungua awali ya pili ya ufungaji kwa wasukuma
 ndinga hao machachari alipofunga bao la nne dhidi ya Schalke 04. Kama ilivyo
 kanuni ya hesabu za pythagoras, Karim alifunga goli hilo kwa kupata usaidizi 
kutoka kwa yule yule aliyempa pasi awali, Cristiano Ronaldo.



Dakika ya 69 ya mchezo, ikawa zamu tena ya Gareth Bale kuutia mpira wavuni baada ya 
kupokea pasi nzuri ya Sergio Ramos. Ubao wa matokeo ukasoma
 Schalke 04 0 Real Madrid 5. Matokeo hayo yalidumu kwa dakika 20 tu
 kwani panapo dakika ya 89 ya mchezo krosi ya Karim Benzema ikamfikia
 Cristiano Ronaldo. Naye hakufanya ajizi, akaitia wavuni na kuwafanya mashabiki wa
 Real Madrid kote ulimwenungi kushangilia kwa tambo na kujidai kwa kila namna.

Dakika iliyofuata, Klaas Jan Huntelaar aliyekuwa tayari amelimwa kadi ya njano
 panapo dakika ya 72, akafunga bao la kuwafutia machozi wenyeji wa mchezo huo.

Kwa matokeo hayo, Schalke 04 inahitaji miujiza ili isonge mbele. Timu hizo 
 zinatarajia kukwaana tena katika mchezo wa pili utakaokimbizwa dimbani 
 Santiago Bernabeu jijini Madrid, Hispania majuma matatu yajayo.

Kwingine barani Ulaya, Galatasaray iliikaribisha Chelsea, vinara wa 
ligi kuu ya Uingereza. Dakika ya 9 tu ya mchezo huo uliopigwa katika
 dimba la Turk Telekom, Fernando Torres akaifungia Chelsea goli la kuongoza.
 Chelsea ikawa timu ya kwanza kutoka Uingereza kufunga goli katika hatua hiyo
 ya 16 ya michuano ya UEFA. Timu zingine kutoka Uingereza, Machester City,
 Arsenal na Manchester United ziliambulia kichapo cha magoli 2-0 kutoka 
 kwa Barcelona, Bayern Munich na Olympiakos.

Chelsea iliendelea kuongoza ikiwa ugenini hadi dakika ya 65 pale Aurelien
 Chedjou alipofunga akisaidiwa na Wesley Sneijer. Matokeo hayo yanaipa ahueni ya
 goli la ugenini Chelsea. Timu hizo zinatarajia kutimuliana vumbi tena wiki tatu zijazo 
pale mitaa ya Fulham, London katika dimba la Stamford Bridge.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog