JAMBO ambalo linaiumiza kichwa Yanga sasa ni kutaka kuhakiki
kama kweli Etoile du Sahel imewasilisha jina la straika, Emmanuel Okwi
kwenye usajili wake kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Lakini katika orodha ya Etoile du Sahel, ambayo
Mwanaspoti imepata nakala yake jana Ijumaa ni kwamba klabu hiyo
imepeleka CAF majina 24 tu, na hakuna jina la Emmanuel Okwi.
Iwapo ikitinga hatua ya makundi ya Ligi ya
Mabingwa Afrika, Etoile inaweza kuongeza majina sita kwani kila klabu
inaruhusiwa kutuma majina 30.
Kwa kifupi ni kwamba, Etoile du Sahel haiwezi
kumtumia Okwi katika Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa Yanga wanaweza
kumtumia raia huyo wa Uganda kwani wametuma jina lake katika shirikisho
hilo mjini Cairo, Misri.
Etoile kwenye usajili wake wa CAF imepeleka wachezaji 24 ambao pia hakuna jina la Okwi.
Waliosajiliwa CAF ni Aymen Mathlouthi, Saif
Ghezal, Ghazi Abderrazzak, Radhouene Felhi, Marouene Tej, Hamza Lahmar,
Alaya Brigui, Baghdad Bounedjah, Abdel Fadel Suanon, Issam Jebali,
Franck Kom, Ahmed Mortadha na Ben Ouannes.
Wengine ni Hamouda Chatti, Marouene Troudi, Hamdi
Nagguez, Aymen Ben Ayoub, Drame Michailou, Mohamed Slama, Zied
Essoussi, Rami Bedoui, Aymen Trabelsi, Fehmi Kacem, Khaled Yahia na
Youssef Mouihb
Ingawa, TFF imesimamisha kwa muda Yanga kumtumia
Okwi, lakini jambo hilo inaelekea linakosa nguvu baada ya Etoile
kuliondoa jina la mchezaji huyo CAF.
Yanga itacheza na Komorozine ya Comoro katika Ligi
ya Mabingwa Afrika mwezi ujao ikianza Dar es Salaam kabla ya kurudiana
Comoro.
Okwi alijiunga na Yanga kwenye usajili wa dirisha
dogo akitokea SC Villa ya Uganda kwa mkataba wa miaka miwili huku
ikidaiwa kuwa alipewa dola 100,000 (Sh 160 milioni).
SC Villa iliruhusiwa na Fifa kumtumia mchezaji
huyo kwa mkataba wa miezi sita wakati sakata la madai ya mishahara na
marupurupu yake Etoile yakifanyiwa kazi.
Mbali na madai ya Okwi kwa Etoile hata Simba ilikuwa ikidai dola 300,000 ambazo haijalipwa mpaka sasa na kesi ipo Fifa.
0 maoni:
Post a Comment