Stori: Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
SIRI nzito imefichuka! Baadhi ya maaskofu na wachungaji (baadhi lakini) wa makanisa ya kilokole nchini wanadaiwa kutumia hirizi ili kujaza waumini, Uwazi limenyetishiwa.
SEHEMU ZINAZOKAA HIZIRI
Kwa mujibu wa mfichua siri huyo, watumishi hao wa Mungu wanaojihusisha na ushirikina wamekuwa wakizifunga hiziri hizo sehemu ya juu ya mkono wa kulia na kufichwa na shati la mikono mirefu ambalo nalo huwa ndani ya koti la suti.
Ikadaiwa kuwa, wengine huficha sehemu ya siri ya nguo ya ndani kulingana na maelekezo ya waganga wanaowatengenezea hirizi hizo.
WAUMINI NAO WANENA
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mapaparazi wetu jijini Dar juzi, baadhi ya waumini wa makanisa hayo ya kiroho walisema wamegundua kuwa, wapo viongozi wa makanisa hayo ambao hutumia nguvu za giza ili kuvuta waumini wengi.
LENGO LA KUTUMIA HIRIZI
Waumini hao ambao walidai wana uhakika kuna watumishi wa Mungu feki wengi siku hizi, walisema maaskofu na wachungaji wanaotumia hiziri wana lengo la kujipatia ‘kondoo’ wengi hivyo kuwa na uhakika wa kukusanya sadaka nyingi.
NI WALE WENYE NIA YA UTAJIRI TU
Habari zaidi zinadai kuwa, watumishi wa Mungu waliotumbukia kwenye ushirikina huo ni wale wanaosaka utajiri tu na neno la Mungu kwao si kitu cha lazima.
Watumishi hao wanadaiwa kusema kwenye madhabahu ya makanisa yao kwamba wameokoka, wanatembea na Bwana Yesu, lakini ndani ya mioyo yao hakuna ulokole wala uinjilisti zaidi ya blaablaa tu.
ROMANI, KKKT, ANGLIKANA WALIA
Ikazidi kudaiwa kuwa, pigo kubwa la kuwepo na kutanuka kwa makanisa ya kiroho nchini ni kwa Romani Katoliki (chini ya Kaldinali Polycarp Pengo) Walutheri, KKKT (chini ya uongozi wa Alex Malasusa) na Anglikana (lililokuwa likiongozwa na Valentine Mokiwa) ambao miaka ya karibuni makanisa yao yamemegwa, baadhi ya waumini wamekimbilia katika makanisa ya kiroho.
Hata hivyo, si waumini wote waliokimbilia kwenye makanisa hayo wapo kwa watumishi wanaodaiwa kutumia hiziri, wengine wapo kwenye makanisa salama.
WATUMISHI WA MUNGU WASAKWA
Kufuatia kufichuka kwa siri hiyo, Uwazi liliwatafuta viongozi mbalimbali wa makanisa nchini ili kuzungumzia madai hayo.
Aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania ambaye sasa ni Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Dk. Valentine Mokiwa alipoulizwa juzi na Uwazi kuhusu kuwepo kwa matumizi ya hirizi kwa baadhi ya watumishi wa Mungu, alisema:
“Watu wanasema kuwa nguvu za giza hutumika katika baadhi ya makanisa ya kiroho, lakini kwa upande wangu sijaujua ukweli wala sijathibitisha kwa sababu ni mambo ya kishetani.
“Siku hizi dini imekuwa kama soko kwani wengi hutumia uongo kanisani kwa lengo la kuwajaza watu.”
Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam, Josephat Gwajima kwa upande wake alisema wingi wa waumini katika makanisa mbalimbali ya kilokole hutokana na huduma nzuri na mafundisho mema yanayotolewa na wasimamizi wa makanisa hayo.
Kwa upande wake Kiongozi wa Kanisa la Huduma ya Maombezi, Mbezi Salasala jijini Dar es Salaam, Nabii Flora Peter alisema mtumishi wa Mungu kutumia hirizi katika kuendesha Neno la Mungu ni dhambi kubwa katika utumishi.
“Mungu hapendi, kama kuna mtu wa namna hiyo basi huyo hafai kuongoza kanisa kwa sababu dini ni imani ya mtu, sasa haiwezekani utumikie mabwana wawili,” alisema Nabii Flora.
Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Magnus Muhiche yeye alisema hajawahi kuona ila anachokijua wingi wa watu katika makanisa ni sawa na biashara.
Askofu John Said wa Kanisa la Victoria lililopo Mabibo External jijini Dar es Salaam alipoulizwa kuhusu hilo hakupenda kuchangia kitu chochote.
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi la Ubungo Kibangu jijini Dar, Lusekelo Anthony ‘Mzee wa Upako’ alipigiwa simu, hakupokea, akatumiwa ujumbe wa simu wa meneno (SMS) hakujibu licha ya ujumbe huo kurudiwa mara mbili kwa saa tofauti.
Mwaka 1993, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel & Bible Fellowship, Zakaria Kakobe alifanya mkutano wa Injili kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi, Gangilonga, Iringa ambapo baadhi ya wachungaji wa makanisa wa mkoa huo walifika kumshuhudia.
Baada ya mkutano kumaliza, wachungaji hao walisikika wakisema kuwa, walifika kwa lengo la kuthibitisha kwa macho yao uvumi ulionea kwamba, Kakobe anatumia hirizi kuhubiri, hasa wakati wa kuponya wagonjwa akiwa ameishika mkononi.
Wachungaji hao walishangaa mpaka mwisho wa mahubiri, Kakobe hakuwa ameshika hirizi na kumpongeza kwamba, kumbe maneno ya watu juu ya mtumishi huyo wa Mungu hayakuwa na ukweli hasa kwa jinsi alivyoliitia jina la Yesu kuponya watu.
0 maoni:
Post a Comment