MISS Tanzania 2006-07, Wema Isaac Sepetu, wikiendi iliyopita aliingia katika kipindi kigumu zaidi katika maisha yake, kwa vile lilikuwa tukio zito kulibeba baada ya kuzimia mara tatu ndani ya saa 7.
Wema ambaye ni nyota wa filamu Tanzania, alizingirwa na maumivu makali, yaliyotokana na kumpoteza mtu anayempenda sana, baba yake mzazi, marehemu Balozi Isaac Abraham Sepetu. Balozi Sepetu, alifikwa na mauti Jumapili iliyopita saa 12 asubuhi, ikiwa ni baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya kisukari na shinikizo la damu ambavyo vilimsababishia kupata ugonjwa wa kupooza viungo (kiharusi). Mzee huyo aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, alifikwa na mauti akiwa katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa. Awali, Balozi Sepetu alitolewa Zanzibar alikokuwa anaishi baada ya kuzidiwa kisha akapelekwa TMJ, alipopata nafuu aliruhusiwa kurejea nyumbani.
Hata hivyo, aliporuhusiwa hakurejeshwa Zanzibar, badala yake alipelekwa kwenye nyumba yake iliyopo Sinza Mori, jijini Dar es Salaam ambako alihudumiwa kwa muda kabla ya afya yake kubadilika na kukimbizwa TMJ ambako mauti yalimfika.
WEMA KUZIMIA
Chanzo chetu kilisema: “Wema bado mdogo, katika maisha yake hakuwahi kupatwa na msiba mkubwa kama huu, kumpoteza baba yake kipenzi, ni jambo zito ndiyo maana mpaka sasa tunaongea ameshazimia mara tatu, yaani anazimia na kurejewa na fahamu.” Jumapili saa 7 mchana baada ya kurejewa na fahamu, alisema: “Nimeumia sana kwani huu ni msiba mkubwa kwangu, Baba yangu alikuwa nguzo imara katika maisha yangu, sikuwahi kufikiria kama ningepata msiba mkubwa kama huu. “Taarifa hizi wakati nazipokea nilijua kama utani lakini yote ni mipango ya Mungu, inaniuma sana,” alisema Wema.
WASIFU MFUPI WA MAREHEMU MZEE SEPETU Balozi Sepetu aliwahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo visiwani Zanzibar, vilevile akawa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, miaka ya 1970 wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mwaka 1982, alteuliwa na Mwalimu Nyerere kuwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi, wadhifa ambao aliendelea kuushikilia mpaka kipindi cha Awamu ya Pili chini ya Rais Alhaj Ali Hassan Mwinyi. Kati ya mwaka 2001 na 2006, Balozi Sepetu alichaguliwa kuwa mbunge katika Bunge la Afrika Mashariki kwa tiketi ya CCM, Zanzibar. Balozi Sepetu aliteuliwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi visiwani humo (Zipa). Machi 27, mwaka huu, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein alimteua Balozi Sepetu kuendelea na wadhifa huo wa Zipa kabla ya mauti kumchukua.
Source: GPL
0 maoni:
Post a Comment