MAKOMANDOO sita wa Jeshi la Marekani, wakiwamo wawili walioshiriki kumuua Kiongozi wa Al Qaeda, Osama bin Laden, wamefanikiwa kumuua kinara wa kundi la Al Shabaab anayedaiwa kupanga mashambulizi ya kigaidi katika jengo la biashara la Westgate mjini Nairobi nchini Kenya mwezi uliopita na kusababisha vifo vya watu 68 na wengine zaidi ya 175 kujeruhiwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, aliyeko ziarani nchini Indonesia, aliwaambia waandishi wa habari jana, kuwa gaidi huyo aliuawa wakati wa mapambano kati yake na makomandoo hao. Hata hivyo, hakumtaja jina.
John Kerry alisema “Jumamosi iliyopita, makamandoo hao wa Marekani, walishambulia nyumba ya kiongozi huyo mjini Barawe, Somalia. Mashambulizi yaliyofanywa na wanajeshi wa kikosi maalumu cha Marekani nchini Libya na Somalia, yanaonyesha dhamira ya Serikali ya Marekani kuwasaka magaidi.”
Alisema kwamba, taarifa za kiintelijensia, zinaonyesha kinara huyo ambaye alikuwa mshirika mkuu wa Kundi la Al-Shabaab, alihusika moja kwa moja katika shambulio la kigaidi katika jumba la maduka la Westgate.
Kerry alisema kwamba, baada ya kumaliza kazi hiyo, wanajeshi hao waliondoka mjini Barawe na kurudi Marekani.
Ni katika operesheni hii ambapo pia makomandoo wa Marekani walimkamata kiongozi wa Kundi la Al-Qaeda, Anas al Libi katika mji mkuu wa Libya, Tripoli. Anas al-Liby, anahusishwa na matukio mengi makubwa yakiwamo ya kuwavizia watu wenye asili ya Marekani kuwakamata na kuwafanyia vitendo vya kinyama
0 maoni:
Post a Comment