Sunday, July 28, 2013


MZIMU wa serikali tatu bado unaendelea kukitesa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo jana, Katibu Mkuu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipinga tena uwepo wa serikali tatu na kudai kuwa waliotoa maoni hayo ni wazee wanaosubiri kufa. 


Akizungumza jijini Dar es Salaam katika kongamano la Umoja wa Vijana (UVCCM) la kujadili mchakato wa Katiba Mpya, katika ukumbi wa Arnatouglo, Nnauye alisema nia ya serikali tatu ni kuleta matabaka ambayo yatasababisha migogoro.

“Wazee hawa wanaosubiri kufa wanataka kutuletea matabaka, vijana ndio nguvu kazi ya taifa, kitendo cha kuwepo kwa serikali tatu ni kusababisha mgogoro, kwa nini wasingevunja Muungano enzi za ujana wao? Wamenufaika na Muungano kwa kipindi cha miaka 50, sisi vijana wanataka kutuachia mgogoro!”alisema Nnauye.

Nape alisema kuvunjwa kwa Muungano kutasababisha mgogoro mkubwa wa rasimu kutokana na muda ambao Muungano huo umedumu.

Alisema kuundwa kwa serikali tatu si sera ya CCM kama wanavyodai wapinzani, bali ni maoni ya watu waliyoyawasilisha katika ukusanywaji wa maoni ya Rasimu ya Katiba mpya.

“Sera ya CCM ni kuongoza serikali mbili na si tatu, na hii sera tutaendelea kuitetea na kuilinda mpaka mwisho wa dunia, tunachoamini katika chama chetu hatuogopi kutetea sera ambazo tumezitoa wenyewe,” alisema Nnauye.

Alisema ni vyema zikamalizwa kasoro zilipo katika mfumo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na
si kuongeza madaraka yasiyo na tija.

Nape alisema kitendo cha Tume ya Jaji Joseph Warioba kusema imetumia sheria ya mwaka 1964 kuwa kigezo cha kuundwa kwa serikali tatu si sahihi, kutokana na makubaliano ya mwaka huo kwamba ni serikali mbili.

Kiongozi huyo wa CCM pia alishangazwa na kitendo cha Rasimu ya Katiba mpya kutamka wazi idadi ya mikoa pamoja na wilaya ambazo zitatumika katika uchaguzi na kwamba mwenye jukumu hilo ni Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.

“Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa serikali tatu itaelea katika madaraka, kwani serikali ya Tanganyika itakuwa haiwezi kuwatetea wananchi, hali itakayosababisha kuwepo kwa mgogoro mkubwa wa urasimu ambao ni adui wa maendeleo,” alisema Nnauye.

Aidha alisema kuwa kuvunjika kwa Muungano kutasababisha kuiburuza Serikali ya Zanzibar kiuchumi, kwani asilimia 95 ya uchumi wa visiwani unategemea Tanzania Bara.

Alisema kuwa sera nzuri ya kuwa kiongozi ni kuwatetea wananchi na si kuwazidishia mizigo.

Akizungumzia suala la mgombea binafsi, Nnauye alisema CCM hakiogopi mgombea binafsi, kwani hata akigombea chama hakitapata hasara yoyote.

Nape alisema sera ya CCM ni kukataa wagombea binafsi wanaouza unga na si kukataa mgombea binafsi kama ambavyo vyama vingine vya siasa vinavyodai katika vyombo vya habari.

Alisema katika Rasimu hiyo sura ya 9 inazungumzia umri wa Mbunge kuwa kuanzia miaka 25, lakini kwa CCM suala hilo si sahihi, kwani wabunge wenye miaka 21 wanawajibika vizuri kuliko wazee.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog