Saturday, December 24, 2016


MABINGWA watetezi Tanzania bara Yanga wamelazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa 17 wa Ligi Kuu Soka Tanzania bara dhidi ya African Lyon.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, mabao yalifungwa na Ludovick Venance wa African Lyon na Amis Tambwe kwa upande wa Yanga.
Sare hiyo itaendelea kuibakiza Yanga kwenye nafasi ya pili ikifikisha jumla ya pointi 37 nyuma ya vinara Simba yenye pointi 38.
Matokeo hayo yana faida kwa Simba kama itashinda mchezo wake wa leo dhidi ya JKT Ruvu utakaochezwa kwenye uwanja wa Uhuru, itawaacha wapinzani wake kwa tofauti ya pointi nne kwa kuwa itafikisha pointi 41.
Hata kama Simba itafungwa au kupata sare yoyote bado itaendelea kuongoza.
African Lyon ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza dakika 59 lililofungwa na Venance baada ya kupata krosi nzuri ya Abdallah Mguhi.
Venance aliingia kipindi cha pili dakika 46 kuchukua nafasi ya Awadh Juma.
Aidha, Tambwe akaisawazishia Yanga dakika ya 74 kwa kichwa baada ya kupata krosi ya Juma Abdul.
Kipindi cha kwanza cha mchezo huo kila timu haikuweza kufumumania nyavu ya mwenzake.

Yanga ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga na kushindwa kuzitumia kupitia kwa Tambwe, Haruna Niyonzima, Vicent Bossou, Thaban Kamusoko, Simon Msuva na Geofrey Mwashiuya huku Mguhi kwa upande wa African Lyon akikosa pia.
African Lyon inapata sare ya pili mfululizo na kufikisha pointi 19. Timu hii inazidi kujiwekea rekodi kwa kuzibana timu tatu zinazoongoza ligi, ikitoka kuilazimisha Azam FC sare ya bila kufungana na pia, iliifunga Simba bao 1-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza.

Kikosi cha Yanga kilikuwa na Deogratius Munishi 'Dida', Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Saidi Juma, Simoni Msuva, Thabani Kamusoko/Obrey Chirwa, Amisi Tambwe, Haruna Niyonzima na Deusi Kaseke/Emmanuel Martin.
African Lyon; Jehu Youthe, Miraj Adam, Baraka Jaffary, Halfan Twenye, Hamadi Waziri, Hamadi Manzi, Hassan Isihaka, Omary Abdallah, Awadh Juma/Ludovick Venance, Thomas Maurice na Abdallah Mguhi.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog