Saturday, September 5, 2015


TANZANIA leo inakutana na Nigeria katika mchezo wa Kundi G, kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Saa 10: 30 jioni. Mara ya mwisho Tanzania kukutana na Nigeria ilikuwa Septemba 11, mwaka 2002 katika mechi ya kirafiki na Super Eagles ilishinda 2-0.  Lakini kwenye mechi za mashindano ilikuwa Desemba 20, mwaka 1980, katika mechi za kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia na Taifa Stars ikafungwa 2-0 Uwanja wa Taifa.
Huo ulikuwa mchezo wa marudiano baada ya awali Tanzania kutoa sare ya 1-1 Uwanja wa Surulele mjini Lagos, Nigeria Desemba 6, 1980
Tanzania inakutana na Nigeria leo baada ya miaka 35, je italipa kisasi cha mwaka 1980?
Ahmed Musa (kushoro) na Anthony Ujah (kulia) walikuwepo katika kikosi cha U23 ya Nigeria kilichoitoa Tanzania mwaka 2011


REKODI YA TANZANIA NA NIGERIA

Julai 6, 1972 Mechi ya kirafiki Tanzania 0-0 Nigeria Janauri 12, 1973 Michezo ya Afrika Nigeria 2–1 Tanzania (Surulele, Lagos) Machi 8, 1980 Fainali za Mataifa ya Afrika Nigeria 3–1 Tanzania (Surulele, Lagos) Desemba 6, 1980 kufuzu Kombe la Dunia Nigeria 1- 1 Tanzania (Surulere, Lagos) Desemba 20, 1980 kufuzu Kombe la Dunia  Tanzania 0-2 Nigeria (Uhuru, Dar es Salaam) Sep 11, 2002 Mechi ya kirafiki Nigeria 2-0 Tanzania


Taifa Stars mwaka huo ilikuwa moto wa kuotea mbali, kwani katika Raundi ya Kwanza iliitoa Kenya, Harambee Stars kwa jumla ya mabao 6-3 ikianza kufungwa 3-1 Nairobi Julai 5, mwaka 1980, kabla ya kushinda 5-0 Dar es Salaam Julai 19, 1980. Kwa ujumla mwaka 1980 Tanzania na Nigeria zilikutana mara tatu, pamoja na kwenye mchezo wa Kundi A Fainali za Mataifa ya Afrika Machi 8, 1980 Eagles wakishinda 3–1 Uwanja wa Surulele, Lagos. Mara ya kwanza kabisa Tanzania kukutana na Nigeria ilikuwa katika mchezo wa kirafiki Julai 6, mwaka 1972 na kutoka sare ya 0-0, lakini mechi ya kwanza ya mashindano ilikuwa Janauri 12, mwaka 1973 katika fainali za Michezo ya Afrika.  Nigeria waliokuwa wenyeji ilishinda 2-1 mjini Lagos na kwa bahati mbaya Tanzania ilipoteza mechi zote ikifungwa pia 4-2 na Algeria na 1-0 na Ghana hivyo kushika mkia na Kundi A.
Sunday Oliseh hajawahi kukutana na Tanzania enzi zake anachezea Super Eagles
Faida moja tu katika Michezo ya Afrika mwaka huo ni wachezaji kipa Omar Mahadhi na mshambuliaji Maulid Dilunga (wote sasa marehemu) kuchaguliwa kombaini ya Afrika. Zaidi ya hapo, Tanzania na Nigeria zimekuwa zikikutana katika mechi za kirafiki na kufuzu za vijana tu na leo hatimaye miaka 35 baadaye zinakutana tena katika mchezo wa kufuzu AFCON ya 2017.

MATOKEO YA MECHI 10 ZILIZOPITA ZA TAIFA STARS

Nov 16, 2014: Swaziland 1-1 Tanzania Machi 29, 2015: Tanzania 1-1 Malawi Mei 18, 2015: Tanzania 0-1 Swaziland Mei 20, 2015: Madagascar 2-0 Tanzania Mei 22, 15: Lesotho 1-0 Tanzania Juni 7, 2015: Rwanda 2-0 Tanzania Juni 14, 2015: Misri 3-0 Tanzania Juni 20, 2015: Tanzania 0-3 Uganda Julai 4, 2015: Uganda 1-1 Tanzania Agosti 28, 2015: Tanzania 1-2 Libya
Kocha wa sasa Tanzania, Charles Boniface Mkwasa hakuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Stars timu hizo zilipokutana mara ya mwisho mwaka 1980 na mwaka 2002 alikuwa amekwishastaafu.
Kocha wa sasa Nigeria, Sunday Oliseh alikuwa ndiyo anaibuka kisoka wakati timu hizo zinakutana mara ya mwisho mwaka 1980 na mwaka 2002 licha ya Nigeria kutumia wachezaji wa ligi ya nyumbani pekee, lakini pia alikuwa amekwishastaafu soka ya kimataifa
Lakini Mshauri wa Ufundi wa Taifa Stars, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ alicheza mechi dhidi ya Nigeria kwenye Michezo ya Afrika mwaka 1973. 
Sahau kuhusu historia, Tanzania inakutana na Nigeria ikiwa imetoka kucheza mechi 10 bila kushinda. Mara ya mwisho Taifa Stars ilishinda 4-1 dhidi ya Benin Oktoba 12, mwaka jana Dar es Salaam na tangu hapo imekuwa ikichezea vichapo mfulilizo na kutoa sare.
Safu ya ushambuliaji wa Nigeria leo itawategemea Anthony Ujah aliyesajiliwa na Werder Bremen ya Ujerumani Mei mwaka huu na Ahmad Musa wa CSKA Moscow ya Urusi, ambao walikuwemo kwenye kikosi cha U23 ya nchi yao kilichoitoa Tanzania Juni mwaka 2011.
Tanzania ilifungwa 3-0 mechi ya kwanza Kaduna na Musa na Ujah wote walifunga wakati mchezo wa marudano, Nigeria walipigwa 1-0 bao pekee la Thomas Ulimwengu.
Ulimwengu, Shomary Kapombe na Himid Mao leo wanakutana tena na akina Musa na Ujah Taifa tangu walipokutana mara ya mwisho Juni mwaka 2011.
Charles Boniface Mkwasa hakuwahi kukutana na Nigeria enzi zake anachezea Taifa Stars 

Mkwasa na Oliseh ni makocha wapya walioanza kazi mwezi uliopita baada ya kufukuzwa kwa Stephen Keshi Nigeria na Mholanzi Mart Nooij kwa Tanzania.
Kwa Oliseh huu ni mchezo wa kwanza kabisa kuiongoza Nigeria, wakati Mkwasa atakuwa anaiongoza Tanzania katika mechi ya tatu, baada ya awali kutoa sare ya 1-1 na Uganda mjini Kampala kabla ya kufungwa 2-1 na Libya mjini Kartepe, Uturuki wiki iliyopita.   
Ni Tanzania au Nigeria leo? Dakika 90 zitatoa majibu katika mchezo huo wa kihistoria unaokuja baada ya miaka 35.
Wachezaji wa sasa Super Eagles wanamkumbuka Thomas Ulimwengu aliwafunga walipokutana naye katika mechi ya U23 mwaka 2011

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog