Saturday, August 1, 2015



Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
IKITAJWA orodha ya wachezaji waliong’ara katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na jina la winga wa kushoto wa Azam FC, Farid Malik Mussa (pichani kulia) likakosekana itakuwa kuna mushkeli.
Farid ameng’ara Kagame ya 2015 inayofikia tamati kesho Dar es Salaam na amekuwa na mchango mkubwa kwa timu yake kufika Fainali, ambako itamenyana na Gor Mahia ya Kenya.
Maamuzi ya Kocha Muingereza Stewart Hall, kutowaorodhesha kwenye kikosi cha Kagame mawinga Brian Majwega na Ramadhani Singano ‘Messi’ yalipata upinzani ndani ya uongozi wa Azam FC awali.
Lakini sasa yamekuwa maamuzi ambayo yameleta faraja kwenye timu, kwani dogo aliyepandishwa kutoka akademi ya Azam FC mwaka juzi, Farid amefanya watu wasahau kwa muda kuhusu Majwega na Messi.
Farid amecheza vizuri kule kushoto na amekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia timu kupata mabao kabla ya kufunga bao pekee la ushindi katika mchezo wa Nusu Fainali dhidi ya KCCA jana. 
Na ukitazama wachezaji wa kushoto wa timu nyingine zilizoshiriki mashindano haya hadi sasa, anaweza akapatikana wa kumzidi Farid kwa urefu, mwili na umri- lakini si uwezo.
Farid Mussa akimuacha chini beki wa Yanga SC, Juma Abdul katika mchezo wa Robo Fainali Kombe la Kagame

 

Farid ameonyesha uwezo mkubwa katika mashindano haya hadi sasa, kasi yake, uwezo wa kumiliki mpira, kupiga chenga, akili na maarifa ambayo yanamfanya awe na maamuzi sahihi wakati wote.
Si winga ‘mambio akili sifuri’ kama mawinga wetu wengi wa sasa nchini, huyu ni ‘winga maujuzi’, ambaye anapomtoroka beki anafahamu anakwenda wapi na akifika hapo atafanya nini.
Farid anamchukua beki anamburuza, akifika karibu na kona anainua shingo anaangalia pale ndani wenzake wamekaa vipi, akiona hawajajipanga vizuri, anaingia ndani zaidi kuwavuta.
Ndiyo sababu krosi zake nyingi husaidia Azam FC kupata bao au kusababisha kizaazaa kwenye lango la wapinzani.
Farid kwa sasa ni tishio kwa mabeki na wachezaji mbalimbali wamemzungumzia kama winga bora wa Kagame 2015.
Kesho Saa 10:00 jioni Kombe la Kagame litafikia tamati kwa mchezo wa Fainali kati ya Azam FC na Gor Mahia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Bila shaka itakuwa ni siku nyingine ya kuendelea kushuhudia ubora wa Farid.

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog