Thursday, August 13, 2015


FIFA Leo imetoa tamko la kumzodoa Meneja wa Chelsea Jose Mourinho baada kumtupa nje kusimamia Timu ya Kwanza Dokta wao Mwanama Eva Carneiro kwa kuingia Uwanjani kumtibu Mchezaji alieumia.
Profesa Jiri Dvorak, Daktari Mkuu wa FIFA, ametamka kuwa Mameneja hawana haki yeyote kuwaambia Matabibu wao waingie Uwanjani au la kumtibu Mchezaji alieumia kwani jukumu hilo ni la Dokta aliepo Uwanjani.

Jumamosi iliyopita Uwanjani Stamford Bridge Dokta Carneiro na Tabibu wa Viungo Jon Fearn waliingia Uwanjani kumtibu Eden Hazard kwenye Dakika za Majeruhi wakati Chelsea ipo 2-2 na Swansea City huku wakiwa Mtu 10 baada ya mapema Kipa wao Thibaut Courtois kutolewa nje kwa Kadi Nyekundu.
Kitendo hicho kilimkera Mourinho kwani Mchezaji akihudumiwa na Madokta basi huwajibika kutoka nje ya Uwanja na husubiri amri ya Refa kuingia tena huku Gemu ikiendelea na hilo liliiacha Chelsea iwe Mtu 9 kwa Dakika kadhaa.

Ingawa Dokta Carneiro na Msaidizi wake waliingia Uwanjani baada ya ishara ya Refa na pia kuitwa na Hazard mwenyewe, baada ya Mechi, akiongea kwenye TV, Mourinho alimponda Dokta huyo bila simile na kumsema hajui mchezo unakwendaje.
Kisha zikaibuka ripoti kuwa Mourinho ameamua kumzuia Dokta Carneiro kuhudhuria Mechi na Mazoezi ya Timu ya Kwanza ya Chelsea.
Jambo hilo limezua mjadala mkubwa huko England na wengi kumponda Mourinho.
Leo, Profesa Dvorak amesema Meneja hana wajibu wowote Mchezaji akiumia: “Kitaaluma, kitabibu, Meneja hana sauti. Hiyo ndio Sheria yetu Kitaaluma, na wajibu wetu kimaadili, kumwangalia Mchezaji tu.”
Profesa Dvorak pia ametamka Daktari ni lazima awe Benchi na anaruhusiwa kuingia Uwanjani hata bila ya ridhaa ya Refa kama akiona Mchezaji amekumbwa na tatizo la moyo au ameumia kichwani au amepoteza fahamu.
Profesa Dvorak amenena: “Hapo ni uamuzi wake Dokta na FIFA Siku zote itamuunga mkono.”

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog