Donald Ngoma aliyesajiliwa Yanga SC mwezi uliopita kutoka FC Platinum ya kwao Zimbabwe anatarajiwa kuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Azam FC kesho |
WAKATI kesho Azam FC na Yanga SC zinakutana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, mchezo huo umekuwa gumzo kubwa.
Hiyo itakuwa mara ya pili, Yanga SC na Azam FC kukutana katika Kombe la Kagame, baada ya mwaka 2012 kukutana katika fainali pale pale Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.
Ilikuwa Julai 28, mwaka 2012 katika mchezo uliochezeshwa na refa Thierry Nkurunziza wa Burundi, Yanga SC ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 wafungaji Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 44 na Said Bahanunzi ‘Spider Man’ dakika ya 90 na ushei.
Moja kati ya mambo yanayozungumzwa sana kuelekea mchezo huo ni juu ya mshambuliaji mpya wa Yanga SC, Mzimbabwe Donald Ngoma aliyesajiliwa mwezi uliopita kutoka Platinum FC ya kwao.
Katika mechi nne ambazo Ngoma ameichezea Yanga SC hadi sasa amefunga mabao matatu, mawili katika mechi za kirafiki moja katika Kombe la Kagame.
Lakini Ngoma ameonyesha ni mshambuliaji mpya hatari kwa mabeki kwenye safu ya mbele ya Yanga SC, kwani ana kasi, nguvu na uwezo wa kumiliki mpira.
Anarukia mipira ya juu, ana nguvu akiwa hewani kiasi kwamba ni vigumu mabeki kumdhibiti- huo ni mtihani haswa kwa safu ya ulinzi ya Azam FC kesho.
Bahati mbaya, Ngoma ameonyesha ni mchezaji mwenye hasira, baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wa kwanza tu dhidi ya Gor Mahia na kuponza timu yake kulala 2-1.
Ilikuwa ni kadi ya pili ya njano, baada ya kumsukuma kwa nguvu kama anapiga ngumi mchezaji wa Gor Mahia, aliyetaka kumtumia kama ngao ya kuinuka baada ya wote wawili kuangukia nje ya Uwanja wakati wakigombea mpira.
Na katika mechi kubwa kama hizi, wachezaji wengine huwafanyia wachezaji wa timu pinzani mambo ya kuudhi na yenye kuzalisha hasira.
Kama wachezaji wa Azam FC watafanya mpango wa kumtia hasira Ngoma arudie makosa ya kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya Gor, utakuwa mtihani kwa Mzimbabwe huo.
Yote kwa yote, Ngoma ni mchezaji ambaye hata benchi la Ufundi la Azam FC chini ya kocha Mkuu, Muingereza Stewart Hall linajua ni hatari.
Lakini je, Ngoma ataweza kuupenya ukuta wa Azam FC, ambao hadi sasa haujaruhusu bao hata moja katika mashindano haya? Bila shaka dakika 90 za mchezo wa kesho zitatoa majibu.
0 maoni:
Post a Comment