TIMU ya Taifa ya Tanzania chini
ya kocha mkuu, Mholanzi, Mart Nooij inatarajia kujipima ubavu katika
mechi ya kimataifa ya kirafiki jioni ya leo kwenye uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam dhidi ya timu ya Taifa ya Malawi (The Flames)
kuanzia majira ya saa 11:00 jioni.
Taifa Stars iliyopiga kambi yake
mjini Tukuyu jijini Mbeya inatarajia kuwasili asuhubi hii majira ya saa
4:00 katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa
ndege ya Air Tanzania.
Wapinzani wa Taifa stars tayari
wapo jijini Dar es salaam kwa ajili ya mechi hiyo muhimu kwa makocha
kuangalia uimara wa timu zao kabla ya kwenda kucheza mechi za
mashindano.
Stars na Malawi wanakutana kwa
mara ya pili ndani ya mwezi mmoja kwani mei 4 mwaka huu walipambana tena
katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kutoka suluhu pacha ya bila
kufungana.
Mechi hii itatumika na kocha mkuu
wa Taifa stars, Nooij, kuangalia kama kuna maboresho katika kikosi
chake kinachojiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya Zimbabwe mjini
Harare.
Mechi ya kwanza jijini Dar es
salaam ambayo Stars ilishinda kwa bao 1-0 la John Bocco `Adebayor`, safu
ya kiungo ilionekana kupwaya sana, hivyo leo hii itakuwa nafasi ya
kocha kuona kama viungo wake wameimarika.
Pia safu ya ushambuliaji
ilionekana kukosa nafasi muhimu za kufunga na kwa muda wote walipokuwa
Tukuyu, Nooij alikuwa anahangaika kunoa makali ya washambuliaji wake.
Malawi (Flames) inayonolewa na
mchezaji wake wa zamani Young Chidmozi nayo itakuwa inacheza mechi ya
mwisho ya majaribio kabla ya kwenda N’djamena kuikabili Chad.
Shirkisho la soka Tanzania, TFF kupitia kwa Afisa habari
wake, Boniface Wambura Mgoyo limewataka watanzania kujitokeza kwa wingi
kuishangilia timu yao ambayo kwa sasa inajengwa upya.
Wambura alitaja kiingilio katika
mechi hiyo kuwa kitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu
na kijani. Kwa upande wa VIP B na C kiingilio kitakuwa sh. 10,000 wakati
kwa VIP A itakuwa ni sh. 20,000.
0 maoni:
Post a Comment