Baada
ya kusimamishwa kwa takriban wiki moja, vipindi vya Televisheni vya
shindano la Maisha Plus, vinatarajiwa kurudi tena hewani leo saa tatu
usiku, kupitia kituo cha televisheni kile kile, TBC1.
Akizungumza mapema asubuhi hii katika mkutano na wanahabari, Mratibu
wa shindano hilo ambalo mwaka huu limepewa jina la Maisha Plus
Rekebisha, Ally Masoud `Kipanya', amesema baada ya kukaa chini na
uongozi wa televisheni hiyo, wamekubaliana kimsingi kutangaza ratiba
itakayokuwa rasmi ambayo haitabadilika kama ilivyokuwa awali.
Uongozi wa Maisha Plus ulilazimika kusitisha matangazo ya kipindi
hicho kutokana na kutokuwa na ratiba ya kueleweka ya vipindi hivyo na
kusababisha wapenzi wa kipindi hicho kukosa muda maalum wa kuona
matangazo.
Kipanya amesema ratiba ya vipindi itaanza upya na ratiba itakuwa
kwamba, siku za ijumaa na jumamosi, vipindi vitaoneshwa kuanzia saa tatu
usiku lakini siku zote za wiki zilizobaki, kipindi kitakuwa kinaruka
saa nne na dakika tano usiku.
Alisema vipindi hivyo vitaonyesha hatua za awali ambazo ni usaili na
mpaka kupatikana kwa washiriki 30 waliobahatika kuingia kijijini.
“Tutaanza kuwaonyesha kipindi chetu kuanzia leo hii saa tatu usiku,
kipindi kitaanza kwa kuonyesha hatua za mwanzo kabisa za mashindano
haya,” alisema Kipanya.
Alifafanua akisema kuwa vipindi 10 vya mwanzo vitaonyesha mchakato
mzima wa upatikanaji wa vijana 18 kutoka Tanzania watakao ungana na
vijana wengine 12 kutoka Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi zitakazotoa
washiriki watatu kwa kila nchi.
Usaili wa mwaka huu ulikuwa tofauti na miaka mingine ambapo orodha ya
washiriki 40 ilitengenezwa na ikagawanywa katika makundi mawili ambapo
kundi la kwanza lilikwenda mkoani iringa kuishi kwenye vijiji vya huko
na kushiriki shughuli za kijamii.
Kundi la Pili litaenda visiwani Zanzibar ambalo pia litashiriki
utamaduni wa kila siku wa kimaisha wa visiwani humo ambapo ni washiriki
tisa tu katika kila kundi watachukuliwa na watachujwa kutokana na jinsi
walivyoyamudu maisha ya huko.
“Vijana
wakiwa huko katika vijiji vya kweli watakuwa wakishiriki shughuli za
kilimo, usafi, za kiafya na nyinginezo kabla hawajaingia katika kijiji
cha Maisha Plus”, alifafanua Kipanya.
Baada ya kundi la kwanza na la pili kutoa washiriki tisa kila kundi,
washiriki 18 watakuwa wameshapatikana, na sasa nchi za zikishapata
washiriki wake 12, idadi ya washiriki 30 itaingia kijijini cha Maisha
Plus katikati ya mwezi huu.
0 maoni:
Post a Comment