Monday, February 10, 2014

apigwa_ad02a.jpg
Mchumi wa CCM, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Shadrack Mwanjuguja akidhibitiwa na vijana baada ya kutokea vurugu jana asubuhi katika Kijiji cha Ruanda2 wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Santilya, Mbeya Vijijini. Picha ndogo ni Mkuu wa Polisi Kituo cha Kati, Mbeya, Richard Mchomvu akimsindikiza hospitali Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Mchungaji Lackson Mwanjale baada ya kujeruhiwa katika kata hiyo. 
Mikoani. Wabunge wawili, mmoja wa CCM na mwingine wa Chadema, jana walikula vichapo walipokuwa katika harakati za uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika katika kata 27 nchini.
Wabunge hao, Godbless Lema (Chadema) wa Arusha na Mchungaji Jackson Mwanjele wa Mbeya Vijijini walipata vipigo katika matukio tofauti yanayohusiana na uchaguzi huo.
Lema alidai kuwa alinusurika kifo kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa polisi na ilibidi aanguke chini na kujifanya amezirai ili kujiokoa, katika tukio lililotokea jana jioni, eneo la Shule ya Sombetini alipokuwa akielekea katika kituo cha kupigia kura.
Mara baada ya kufika jirani na kituo cha Sombetini, inadaiwa kuwa polisi walisimamisha gari ya Lema na kuanza kumuhoji lakini ghafla ilitokea kutoelewana kipigo kuanza. Katika tukio hilo, Lema alipata kipigo hadi kuangukia katika mfereji na akiwa chini, alionekana kama amezimia hivyo polisi walimuachia na kuokolewa na wafuasi wa Chadema.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Lema alisema bila kujifanya amezirai angeweza kuuawa... "Wamenipiga sijui kosa langu, mimi kama mbunge niliitwa na mawakala wakiomba gari kubeba masanduku na ni kweli nilikuwa nimewasha taa za gari nikishangilia. Kesho naenda kupimwa hospitali kwani nina maumivu kwenye mbavu. Baada ya hapo nitajua cha kufanya kwani walionipiga nawajua."
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana jana kuelezea tukio hilo lakini mmoja wa polisi waliokuwa eneo la vurugu hizo, alisema walilazimika kimdhibiti Lema, kwani alikuwa anafanya fujo jirani na kituo cha kura.
"Hakuna aliyempiga, alianguka mwenyewe kwenye mfereji, tulimtaka aondoke kwa amani akagoma," alisema askari huyo.
Mbeya Vijijini
Mchungaji Mwanjale kwa upande wake, aliumizwa baada ya kupigwa na kundi linalodaiwa kuwa la wafuasi wa Chadema, katika Kitongoji cha Shipongo, Kijiji cha Ruanda, Mbeya wakati yeye na makada wengine wa CCM walipofika hapo wakiwa kwenye gari la chama hicho.
Mbunge huyo alivuja damu nyingi kichwani na mashuhuda wa tukio hilo walisema kabla ya kupigwa, kulikuwa patashika baina ya walinzi wa CCM na wale wa Chadema waliokuwa wakilinda kura katika uchaguzi huo.
Mchungaji Mwanjale inaelezwa kuwa alijiokoa baada ya vijana hao walipomwacha na kuanza kumshambulia Mchumi wa CCM, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Shadrack Mwanjuguja ambaye alikuwa amefuatana naye.
Baada ya kuponyoka, Mwanjale alikimbilia kwenye nyumba moja iliyopo karibu na vijana hao walimfuata na kugonga kwa nguvu ili waingie ndani, lakini alitoroka kupitia mlango wa nyuma kisha kuruka uzio wa nyumba hiyo huku Mwanjuguja akiwekwa chini ya ulinzi.
Mbunge huyo na mwenzake waliokolewa na polisi wa doria waliokuwa wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) Mbeya, Richard Mchomvu ambaye aliwachukua na kuwapeleka Kituo cha Afya Kilembo kwa ajili ya matibabu.
Daktari wa kituo hicho, Franco Anthony alisema Mchungaji Mwanjale alipigwa na kitu kizito kichwani na kushonwa nyuzi tatu huku mwenzake Mwanjuguja akishonwa nyuzi mbili kichwani.
Baada ya kupata matibabu walikwenda Kituo cha Polisi Mbalizi kufungua jalada la mashtaka. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema watu saba walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.
Vurugu Bagamoyo
Vurugu ziliibuka katika uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Magomeni, Bagamoyo na kusababisha polisi kutumia mabomu ya machozi baada ya watu wanaodhaniwa ni wafuasi wa vyama vya CUF na Chadema kuwashambulia wa CCM.
Katika vurugu hizo zilizotokea saa mbili asubuhi, inadaiwa zaidi ya wafuasi 15 wa CCM walijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba kuwa watu kadhaa walikamatwa huku polisi wakiendelea na uchunguzi.
Lindi
Msimamizi wa Uchaguzi Kata ya Namikago, Wilaya ya Nachingwea, Valery Kwembe alimtangaza Alferd Mhagama wa CCM kuwa mshindi kwa kura 511 dhidi ya Hamisi Chingole wa Chadema (188), Hamis Malipiche wa CUF (110) na Belisimas Mbinga wa ADC (1).
Katika Kata ya Kiwalala CCM imeibuka mshindi baada ya Sheneni Zahoro kupata kura 1,158 akifuatiwa na wa CUF, Shazil Mosha 803 na Mboga Hassan wa Chadema 90.
Moshi
Katika Kata ya Kiborloni, Moshi, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Erasmo Silayo alimtangaza Frank Kagoma wa Chadema kuwa mshindi kwa kupata kura 1,019 dhidi ya 255 za Willy Tulli wa CCM. Mgombea wa UDP, Aidan Mzava aliambulia kura mbili. chanzo MWANANCHI

0 maoni:

Post a Comment

waliotembelea blog