MASHABIKI wa Liverpool huenda wakachekelea kwa
muda kukalia usukani endapo timu yao itaichapa Cardiff City mchana wa
leo Jumamosi.
Arsenal inaongoza Ligi Kuu England ikiwa na pointi
35 lakini Liverpool na Chelsea itakayocheza keshokutwa Jumatatu na
Arsenal wote wana pointi 33.
Potezea hiyo, ngoma ipo kwenye Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam jioni hii. Kuna mechi matata ya Nani Mtani Jembe
kati ya Simba na Yanga ambao ni mchezo wa kujifurahisha lakini uliobeba
uzito wa aina yake kishabiki.
Simba inashuka uwanjani ikijivunia majembe yake
mapya ambayo ni makipa, Yaw Berko, Ivo Mapunda, kiungo, Awadhi Juma,
straika Ally Badru na beki Donald Musoti lakini kama haitoshi, Wekundu
hao wana kocha mtaalamu na mwenye mbwembwe za aina yake Zdravko
Logarusic kutoka Croatia.
Ndani ya kambi ya Simba mjini Zanzibar mambo
yalikuwa shwari wiki nzima huku wakipigishwa tizi mara mbili kwenye
Uwanja wa Fuoni.
Rudi kwa Yanga, ina vifaa vipya matata kama Juma
Kaseja, Hassan Dilunga na straika aliyezua gumzo zaidi nchini baada ya
kutua Jangwani, Emmanuel Okwi.
Timu hizo mbili zinakumbana zikiwa na wachezaji
ambao wamewahi kuzichezea zote kwa nyakati tofauti jambo ambalo ni
burudani nyingine.
Wachezaji hao kwa upande wa Yanga ni Juma Kaseja,
Kelvin Yondani, Mrisho Ngassa, Ally Mustapha ‘Barthez’, Deo Munishi
‘Dida’, Athuman Idd na Okwi. Simba ina makipa Mapunda na Berko na Amri
Kiemba.
KOCHA YANGA
Ernest Brandts ambaye ni kocha wa Yanga alisema;
“Tumejiandaa vizuri na sasa tumebakiza dakika chache kabla ya mechi.
Kiujumla timu ipo vizuri na majeruhi tuliyenaye ni Salum Telela pekee
ambaye hayuko vizuri sana.”
“Ninachowaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja
kushabikia timu yao na naamini tutashinda mchezo huo bila
shida,”alisema kocha huyo kwa kujiamini huku akikiri kwamba anaweza
kumtumia Okwi dakika kadhaa.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’
alisema; “Tuna kila sababu ya kushinda mchezo huo, maandalizi yalikuwa
mazuri na kila kitu kinakwenda sawa.”
0 maoni:
Post a Comment