Tanzania ikitajwa kuwa ni miongoni mwa nchi zenye amani na
utulivu, imebainika kuwa Watanzania ni miongoni mwa watu wasio na furaha
na waliokata tamaa hapa duniani.
Ripoti inayoonyesha orodha ya nchi zenye furaha
duniani ya mwaka 2013 (World Happiness Report 2013), imeitaja Tanzania
kuwa ni miongoni mwa nchi 10 za mwisho duniani kati ya nchi 156
zilizofanyiwa utafiti huo.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa na kundi la wataalamu
kutoka Umoja wa Mataifa (UN), kati ya mwaka 2010 na 2012, inaonyesha
kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 151 ikiburuta mkia pamoja na nchi za
Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Benin na Togo.
Upatikanaji wa huduma za jamii, mtazamo wa watu
kuhusu rushwa, umri wa kuishi, ukosefu wa kazi, pato la taifa na ukarimu
wa watu katika nchi husika, ni baadhi ya vigezo vilivyoangaliwa wakati
wa kuandaa taarifa hiyo.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alieleza
kushtushwa na ripoti hiyo kwa maelezo kwamba ni asilimia 11.7 tu ya
Watanzania wasio na ajira na kwamba wale wanaofanya kazi, wanapata
huduma zote za msingi, ikiwa ni pamoja na kwenda likizo na mishahara
inayolingana na taaluma zao.
“Watanzania wana furaha, kwa upande wa wafanyakazi
wanapata haki zao zote wanazostahili, sijui ni vigezo vipi
wametumia…kwa mujibu wa takwimu za 2006 ni asilimia 11.7 ya Watanzania
ndio waliokuwa hawana kazi, lakini wakati huo idadi ya watu ilikuwa
ndogo, hivi sasa imeongezeka,” alisema Kabaka na kuongeza:“Usafiri ndiyo
tatizo linalowasumbua wafanyakazi wengi kwa kuwa wanachelewa kwenda
kazini.”
Naye, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Salum alisema
pamoja na vigezo vingine vilivyotumika kutambua furaha ya Watanzania,
umaskini ndiyo unaoweza kuwa chanzo cha Tanzania kushika nafasi za
mwisho.
“Inategemea na vigezo vingine walivyovitumia,
nakubali kuwa Tanzania ni maskini pengine hali hiyo imeifanya nchi
kushika nafasi ya mwisho,” alisema Salum.
Nchi zilizoongoza
Taarifa hiyo imezitaja nchi tano; Denmark, Norway,
Uswisi, Netherlands na Sweden kuwa ndizo zinazoongoza kwa watu wake
kuwa na furaha zaidi duniani, huku Angola ikishika nafasi ya kwanza
Afrika na ya 61 duniani ikifuatiwa na Algeria (73), Libya (78), Ghana
(86), Zambia (91), Lesotho (98), Morocco (99) na Swaziland (100).
Kwa upande wa Afrika Mashariki, wananchi wa Uganda
ndio walionekana kuwa na furaha zaidi kwani nchi hiyo imeshika nafasi
ya 120 wakifuatiwa na Kenya (123), Tanzania (151), Rwanda (152) na
Burundi (153).
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kati ya mwaka 2005 na
2012, nchi 60 duniani ziliongeza viwango vya furaha kwa watu wake, kati
ya hizo 16 zikiwa barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.
0 maoni:
Post a Comment