RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Makamu wake, William Ruto, sasa wanakabiliwa na shinikizo la kutakiwa kujiuzulu, kutokana na shambulio la kigaidi kwenye maduka ya Westgate.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwako kwa habari kwamba viongozi hao wa juu pamoja na serikali kwa ujumla walikuwa na taarifa za kutokea kwa shambulio hilo kabla halijatekelezwa Septemba 21, mwaka huu.
Tayari taasisi na watu wa kada mbalimbali nchini Kenya wamewataka viongozi hao kuwajibika kutokana na kile walichodai kuwa walishindwa kuchukua hatua kuzuia tukio hilo, licha ya taarifa za kutosha walizokuwa nazo.
Shinikizo hilo limekuja baada ya ripoti ya kiintelijensia yenye jumla la maneno 8,800 kunaswa na vyombo vya habari nchini Kenya, ikielezea taarifa zote za kutokea kwa tukio la kigaidi kati ya Septemba 13 na 21.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais Kenyatta, Makamu wake Ruto, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (NIS) Brigedia Michael Gichangi, Waziri wa Mambo ya Ndani Joseph Lenku, wote walikuwa na taarifa za kutokea kwa shambulio hilo.
Ni taarifa hizo ndizo ambazo zimeushtua umma wa Kenya, ambapo hivi karibuni taasisi zisizo za kiserikali, ikiwamo ile inayoongozwa na Okiya Omutata zimetishia kuwaongoza Wakenya kuingia mtaani kuwaondoa madarakani Rais Kenyatta na Makamu wake endapo hawatawajibika wao wenyewe.
Mbali na hilo, taarifa za sasa za Al-Shabaab kudai kuwa walizungumza na Rais Uhuru Kenyatta na kumpa onyo la kufanya shambulizi la kigaidi nchini mwake ndizo zilizoamsha hasira za Wakenya wengi, kwamba kiongozi huyo anaujua ukweli halisi kuhusu tukio hilo.
Kupitia akaunti yao ya twitter, ambayo ilifungwa baada ya shambulio la Westgate, lakini ilifunguliwa tena hivi karibuni, Al-Shabaab walidai kuwa katika mazungumzo yao hayo na Rais Kenyatta, walimuonya juu ya uwezekano wa kufanya shambulio la kigaidi Westgate au kwenye Bunge la nchi hiyo.
Katika ujumbe wao huo wa kwenye twitter, Al-shabab walichapisha mazungumzo baina yao na yule waliyedai Rais Uhuru Kenyatta.
Wiki iliyopita, gazeti la Standard lilikariri ripoti ya siri ya Intelijensia yenye namba 184/2012 iliyowasilishwa Septemba 21, 2012, ambayo ilikuwa ikieleza juu ya kuwako kwa mipango ya siri ya magaidi kutekeleza shambulio katika ardhi ya Kenya.
Ripoti hiyo ilieleza juu ya kuwako kwa watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni magaidi, waliokuwa wametua Nairobi wakipanga shambulio la kujitoa mhanga katika tarehe ambazo hazikujulikana.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, washirika wa Al Shabaab, wako Nairobi wakiwa na mpango wa kutekeleza shambulizi la kujitoa mhanga, wakilenga Westgate Mall na Holy Family Basilica.
Ripoti hiyo iliwataja Sheikh Abdiwelli Mohamed, Sheikh Hussein na Sheikh Hassan kuwa wanaaminiwa kumiliki ‘Vest’ mbili za kujitoa mhanga, mabomu 12 ya kurushwa kwa mkono na bunduki mbili aina ya Ak 47 na kwamba tayari walikuwa wameandaa maeneo ya kutekeleza mashambulizi.
“Magaidi wamekuwa chini ya usaidizi wa Sheikh Hassan, maarufu kwa jina la Blackie wa Majengo na Omar Ali, maarufu kwa jina la Jerry, ambao wanaishi karibu na kituo cha mafuta cha Mamba na Huruma Mosque, pembezoni mwa barabara ya Juja,” Gazeti hilo lilikariri sehemu ya ripoti hiyo ya NIS.
Pia ripoti hiyo ya NIS ilionesha kwamba watu wawili wanaosadikiwa ni magaidi wenye asili ya Kisomali kutoka kikundi cha Al Shabab waliingia Sudan Kusini kwa kupitia Djibouti, Eritrea na Sudan, kisha Uganda, kabla ya kutumia mpaka wa Busia au Malaba kuingia nchini Kenya.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Standard, ripoti hiyo ilieleza kwamba, magaidi hao walisaidiwa na Teskalem Teklemaryan, ambaye ni mwandishi anayeishi nchini Uganda na Sudan Kusini.
Kwamba wawili hao walikuwa wamebeba bunduki moja ya kivita aina ya GPMG, mabomu manne ya machozi, mkanda mmoja wa risasi, bunduki tano aina ya AK 47, vazi la kuzuia risasi ambalo namba yake haijulikani na ramani mbalimbali za mji wa Nairobi.
Ripoti hiyo ilifafanua kwamba, Maalim Khalid, maarufu kwa jina la Maalim Kenya, ambaye anahusishwa na matukio ya milipuko mbalimbali ya mabomu, anatambulika kama mkuu wa mipango ya kigaidi nchini Kenya.
Maalim Khalid alielezewa katika ripoti hiyo ya NIS kwamba alihusika na shambulizi la kigaidi katika kituo cha Mchakos, Jengo la Assanands na Bellavista Club mjini Mombasa.
Pia ripoti hiyo inamhusisha Maalim Khalid na mpango wa kuteua vijana 20 wa Kenya ambao aliwapeleka katika miji ya Mark na Barawe, kwa ajili ya kupewa mafunzo ya kigaidi.
Kuvuja kwa taarifa hizo kulikuja ikiwa ni siku chache tangu kutekelezwa kwa shambulio la kigaidi lilioua watu zaidi ya 67 katika maduka ya Westgate.
Kamati ya Bunge inayohusika na masuala ya usalama, ilikwishamuweka kitimoto Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa Kenya (NIS), Jenerali Michael Gichangi, ili aeleze kama kuna uzembe wa kiusalama uliosababisha magaidi hao kutimiza azima yao.
Wabunge wa nchi hiyo wanaamini kwamba kulikuwa na upungufu ndani ya Idara ya Upelelezi ya Usalama wa Taifa, hali ambayo iliruhusu magaidi kupanga na kutekeleza shambulizi la Westgate Mall.
0 maoni:
Post a Comment